MUHTASARI WA HOTUBA YA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, MHE. UMMY A. MWALIMU (MB) KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2019/2020


MUHTASARI WA HOTUBA YA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, MHE. UMMY A. MWALIMU (MB) KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2019/2020
A. UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ndani ya Bunge lako Tukufu, ambayo imechambua Bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ninaomba kutoa hoja sasa ili Bunge lako likubali kupokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Kazi za Wizara kwa mwaka 2018/19 na Vipaumbele vya Wizara kwa mwaka 2019/20. Aidha, ninaliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Kawaida pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa mwaka 2019/20.
2. Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu siku ya leo na kuwasilisha hotuba ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Aidha, ninapenda kutumia fursa hii kwa heshima na unyenyekevu mkubwa kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake imara na pia kwa dhamira yake, maono yake na udhubutu wake ambao umekuwa dira sahihi katika utendaji wangu na katika kuimarisha utoaji wa huduma za Afya, Ustawi na Maendeleo ya Jamii nchini. Ni dhahiri kuwa katika kipindi kifupi cha miaka mitatu ya uongozi wake Watanzania wameshuhudia mageuzi makubwa katika utoaji wa huduma za afya nchini ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya afya katika halmashauri na mikoa mbalimbali nchini, kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na huduma za matibabu ya kibingwa. Ninamuahidi Mheshimiwa Rais kuwa Wizara itaendelea kubuni na kutekeleza mikakati mbalimbali ili kuhakikisha huduma za afya nchini zinawafikia watanzania walio wengi hususan wenye kipato cha chini.
3. Mheshimiwa Spika, ninapenda kutoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele katika jitihada za kuboresha huduma za afya hususan zinazohusu Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, Lishe, mapambano dhidi ya Kifua Kikuu sambamba na kuhimiza usawa wa jinsia na uwezeshaji wa wanawake na kuzingatia haki za mtoto katika jamii yetu.
4. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kumshukuru Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake mahiri unaosaidia kuleta tija na ufanisi katika utendaji na kuimarisha huduma zinazotolewa katika Sekta ya Afya, Ustawi na Maendeleo ya Jamii. Aidha, ninampongeza kwa hotuba yake aliyoiwasilisha kwenye Bunge lako Tukufu tarehe 4/04/2019 ambayo imetoa dira ya jinsi Serikali itakavyotekeleza majukumu yake katika mwaka 2019/20.
5. Mheshimiwa Spika, ninapenda kukupongeza wewe binafsi kwa kuendelea kutekeleza majukumu yako kwa weledi katika kuliongoza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, ninampongeza Naibu Spika Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson (Mb) katika utekelezaji wa majukumu yake. Vilevile, nitumie fursa hii kuwapongeza Wenyeviti wa Bunge kwa kusimamia vyema mijadala ndani ya Bunge.
6. Mheshimiwa Spika, kipekee ninapenda kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Peter Serukamba (Mb), na Makamu Mwenyekiti, Mheshimiwa Juma Nkamia (Mb) kwa
2
ushauri na maelekezo waliyoyatoa wakati wa maandalizi ya Bajeti hii. Aidha, ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa ushirikiano mzuri wanaonipatia ikiwemo kutoa ushauri na maoni mbalimbali yenye lengo la kuboresha huduma za Afya, Ustawi na Maendeleo ya Jamii. Ninawaahidi kwamba, Wizara yangu itazingatia ushauri wenu na kuendelea kuwapa ushirikiano katika kutekeleza majukumu na kazi zetu za kuwatumikia wananchi ndani na nje ya Bunge.
7. Mheshimiwa Spika, Natoa pole kwako na watanzania wote, waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki zao kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na magonjwa, ajali, majanga pamoja na wahanga wa vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia hususan watoto waliouawa kikatili katika Mkoa wa Njombe na maeneo mengine. Pia natoa pole kwa wagonjwa na majeruhi wa ajali waliopo hospitalini na majumbani. Namuomba Mwenyezi Mungu awaponye haraka ili waweze kuendelea na ujenzi wa Taifa.
8. Mheshimiwa Spika, Baada ya kusema hayo, ninapenda sasa kutoa maelezo kuhusu utekelezaji wa shughuli za Wizara kwa mwaka 2018/19, Vipaumbele vya Wizara kwa mwaka 2019/20 pamoja na maombi ya fedha ambazo zitaiwezesha Wizara yangu kutekeleza majukumu yake.
B. MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI NA MPANGO WA MAENDELEO KWA MWAKA WA FEDHA 2018/19
9. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majukumu yake, Wizara imeendelea kuzingatia Sera, Mipango Mikakati pamoja na makubaliano ya Kitaifa na Kimataifa yenye lengo la kuimarisha utoaji wa huduma za afya nchini, maendeleo ya wanawake na jinsia, haki, ulinzi na ustawi wa watoto na wazee
10. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2017/18, Wizara yangu ilipanga kutekeleza afua mbalimbali zenye lengo la kuboresha utoaji huduma za Afya kama nilivyoanisha katika aya ya 12 ya Hotuba yangu. Hii ikiwa ni pamoja na;
a) Kuimarisha Huduma za Kinga, Tiba, na kuongeza usawa katika kutoa huduma za afya,
b) Kuimarisha huduma za afya ya uzazi na mtoto ili kupunguza vifo vya wanawake wajawazito na watoto,
c) Kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba, vitendanishi na chanjo katika vituo vya kutolea huduma za afya,
d) Kuimarisha matibabu ya kibingwa nchini kwa kuendeleza ujenzi, upanuzi, ukarabati wa miundombinu na kufunga mitambo ya kisasa ya kutolea huduma za afya katika Hospitali za ngazi ya Taifa, Hospitali za Rufaa za Kanda na Hospitali za Rufaa za Mikoa.
11. Mheshimiwa Spika, kupitia Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Wizara ilipanga kutekeleza kazi zifuatazo:
a) Kuimarisha upatikanaji wa haki, maendeleo na ustawi watoto ikiwemo kwa watoto walio katika mkinzano wa Sheria;
b) Kuwezesha wazee wasiojiweza na watoto walio katika mazingira hatarishi kupata huduma za msingi;
c) Kuhamasisha jamii kushiriki katika shughuli za kujiletea maendeleo kwa kuzingatia rasilimali walizonazo;
Mapato na Matumizi ya Fedha Fungu 52 (Idara Kuu ya Afya)
12. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia fungu 52 (Afya) inalo jukumu la kusimamia upatikanaji na utoaji wa huduma za Afya nchini. Wizara hukusanya mapato kutokana na
3
huduma za Tiba zitolewazo na Hospitali zilizo chini yake, tozo za huduma katika Taasisi mbalimbali, Ada za Vyuo na Uuzaji wa Zabuni.
13. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2018/2019, Wizara, Taasisi pamoja na Hospitali zilizo chini yake ilikadiriwa kukusanya kiasi cha Shilingi 308,790,390,402.00 kutoka kwenye Vyanzo mbalimbali vya mapato. Hadi kufikia Machi, 2019 kiasi cha Shilingi 211,295,910,120.31 zilikusanywa sawa na asilimia 68.4 ya lengo la mwaka. Wizara itaendelea kusimamia na kuboresha ukusanyaji wa Maduhuli ya Serikali kwa kuendelea na utaratibu wa kulipia huduma kupitia Benki, uhamasishaji kuhusu kulipa Maduhuli ya Serikali, Udhibiti wa Makusanyo na kuwaongezea watendaji ari ya kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, Uboreshwaji wa Huduma za Bima na Kuimarishwa kwa Mfumo wa Malipo kwa njia ya Ki-elektroniki.
14. Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka 2018/2019, Wizara kupitia fungu 52 (Afya) iliidhinishiwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupokea na kutumia jumla ya Shilingi 866,233,475,000.00. Kati ya fedha hizo kiasi cha Shilingi 304, 473, 476,000.00 sawa na asilimia 35 ya bajeti yote ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida, ambapo Shilingi 87, 514, 048,000.00 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo na Shilingi 216, 959, 428,000.00 ni kwa ajili ya Mishahara ya watumishi.
15. Mheshimiwa Spika, Fedha zilizopitishwa kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo ni Shilingi 561,759,999,000.00 sawa na asilimia 65 ya bajeti yote. Kati ya fedha hizo, jumla ya Shilingi 376, 800,000,000.00 sawa na asilimia 67 ni kutoka Serikali na Shilingi 184,959,999,000.00 sawa na asilimia 33 kutoka kwa Wadau wa Maendeleo wanaochangia Sekta ya Afya kupitia Mfuko wa Afya wa Pamoja (Health Basket Fund), Mfuko wa Dunia wa Kupambana na UKIMWI, TB na Malaria (Global Fund), Benki ya Dunia na wengineo.
16. Mheshimiwa Spika, Hadi kufikia Machi, 2019 Wizara ilipokea jumla ya Shilingi 340,248,966,788.06 ya bajeti iliyoidhinishwa ya Shilingi 866,233,475,000.00 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake. Fedha zilizopokelewa kwa ajili ya matumizi ya kawaida katika kipindi cha Julai 2018 hadi Machi 2019 ni Shilingi 249,194,163,435.96 sawa na asilimia 82 ya fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida kwa mwaka. Kati ya fedha hizo Shilingi 69,581,445,321.74 zilitumika katika matumizi mengineyo (OC) ikiwa ni sawa na asilimia 79.5 ya kiasi kilichotengwa na Shilingi 179,612,718,114.22 zilitumika kulipia mishahara (vote 52) sawa na asilimia 83 ya kiasi cha fedha kilichotengwa.
17. Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa Miradi ya Maendeleo, hadi kufikia Machi 2019 kiasi cha Shilingi 91,054,803,352.10 kilipokelewa, Kati ya fedha hizo, kiasi cha Shilingi 81,361,323,229.82 ni fedha za ndani na Shilingi 9,693,480,122.28 ni fedha za nje zilizopokelewa kupitia mfumo wa “exchequer”. Aidha, Wizara ilipokea jumla ya Shilingi 180,000,000,000.00 kutoka Mfuko wa Dunia wa Kupambana na Malaria, UKIMWI na Kifua Kikuu (Global Fund) nje ya mfumo wa “Exchequer”. Pia, Wizara ilipokea kiasi cha Shilingi 5,100,000,000 ambazo zilipelekwa moja kwa moja OR – TAMISEMI kupitia Mfuko wa Afya wa Pamoja kwa ajili ya ukarabati wa Vituo vya Afya ili viweze kutoa huduma bora za Afya ya uzazi na mtoto. Vilevile, kwa kipindi cha Julai 2018 hadi Machi 2019, Wizara ilipokea jumla ya Shilingi 50,057,739,553.94 kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya kutekeleza afua mbalimbali katika Sekta ya Afya, kati ya fedha hizo kiasi cha shilingi 20,607,365,734.08 ni kwa ajili ya utekelezaji wa Mpango wa Malipo kwa Ufanisi (Results Based Financing - RBF), kiasi cha shilingi 17,757,339,228.38 ni kwa ajili ya kuwajengea uwezo watumishi wa sekta ya Afya na shilingi 11,693,034,591.48 kwa ajili ya mradi wa Maabara ya Jamii ya Afrika Mashariki.
4
18. Mapato na Matumizi ya Fedha – Fungu 53 (Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii)
19. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Wizara kupitia Fungu 53 (Maendeleo ya Jamii), ilitarajia kukusanya kiasi cha Shilingi 3,090,796,000 kutokana na ada za wanafunzi kutoka katika Vyuo nane vya Maendeleo ya Jamii vya Buhare, Uyole, Rungemba, Mlale, Misungwi, Ruaha, Mabughai na Monduli, ada za wanafunzi katika Chuo cha Ustawi wa Jamii Kisangara pamoja na ada za mwaka na faini za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. Hadi kufikia Machi, 2019 Wizara pamoja na Taasisi zake imefanikiwa kukusanya kiasi cha Shilingi 1,493,051,049 sawa na asilimia 48.3 ya makadirio ya mapato.
20. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Wizara (Fungu 53) iliidhinishiwa na Bunge lako Tukufu matumizi ya Shilingi 32,971,821,592.60. Kati ya fedha hizo, Shilingi 28,057,976,592.60 sawa na asilimia 85.1 ya bajeti ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida ambapo Shilingi 12,941,014,592.60 ni fedha za Matumizi Mengineyo na Shilingi 15,116,962,000 ni kwa ajili ya Mishahara. Aidha, Wizara (Fungu 53) iliidhinishiwa Shilingi 4,913,845,000 sawa na asilimia 15 ya bajeti kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo ambapo Shilingi 1,500,000,000 ni fedha za ndani na Shilingi 3,413,845,000 ni fedha za nje.
21. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Machi, 2019 Wizara imepokea jumla ya Shilingi 17,877,260,865.00 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Miradi ya Maendeleo sawa na asilimia 54 ya bajeti iliyoidhinishwa. Kati ya fedha iliyopokelewa, Shilingi 8,007,033,192.60 sawa na asilimia 62 ni Matumizi Mengineyo, Shilingi 8,341,028,627.60 sawa na asilimia 55 ni Mishahara na Shilingi 1,529,199,045.00 sawa na asilimia 31 ya bajeti ya utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo.
C. UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU CHINI YA IDARA KUU YA AFYA
Utekelezaji wa majukumu ya Fungu 52 umeainishwa kuanzia ukurasa wa 16 hadi 95 wa hotuba yangu
HUDUMA ZA KINGA
Chanjo
22. Mheshimiwa Spika, Hadi kufikia Machi 2019, Serikali ilitoa fedha kiasi cha Shilingi bilioni 98.5 kwa ajili ya ununuzi wa chanjo na vifaa vya kutolea chanjo kulingana na mahitaji. Wizara kupitia Mpango wa Taifa wa Chanjo iliweza kutoa huduma za chanjo za watoto chini ya mwaka mmoja kwa kiwango cha asilimia 98 ya lengo. Aidha, Wizara iliendelea na ukarabati wa majengo ya maghala ya kutunzia chanjo yaliyopo Mabibo- Dar es Salaam, kama mkakati wa kuimarisha usambazaji wa chanjo nchini. Vilevile, Wizara kwa kushirikiana na wadau imefanikiwa kununua jumla ya majokofu yanayotumia nguvu ya jua 1,385 yenye thamani ya Shilingi bilioni 13.9 yaliyosambazwa katika Halmashauri zenye uhitaji katika mikoa 14 ambayo ni; Dodoma, Geita, Kigoma, Kagera, Lindi, Tanga, Mtwara, Mbeya, Shinyanga, Songwe, Singida, Mara, Mwanza na Pwani kwa lengo la kutunzia chanjo na kusogeza huduma za chanjo karibu na Jamii.
Afya na Usafi wa Mazingira
23. Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha Julai 2018 hadi Machi 2019, Wizara iliendelea kutekeleza Kampeni yenye lengo la kuhimiza ujenzi na matumizi ya vyoo bora inayojulikana kama“USICHUKULIE POA NYUMBA NI CHOO” ambapo mikutano ya uhamasishaji jamii imefanyika katika Mikoa ya Morogoro, Tanga, Mbeya, Songwe na Dodoma. Wizara imeendelea kudhibiti kuingia kwa magonjwa ya kuambukiza yenye hatari ya kusambaa Kimataifa ukiwemo ugonjwa wa Homa ya Manjano kupitia maeneo ya mipakani kwa kufanya ukaguzi wa wasafiri wanaotoka katika nchi zenye
5
maambukizi. Aidha, Wizara imeimarisha huduma ya chanjo katika vituo vya afya mipakani ikiwemo kuanza kutoa huduma hiyo katika Bandari ya Mtwara na Hospitali ya Rufaa Dodoma.
24. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha utayari wa kukabiliana na tishio la mlipuko wa Ugonjwa wa Ebola ambao unaendelea nchini DRC, Wizara imenunua na kusambaza vipimajoto 106 (Handheld and Walkthrough thermal Scanners) kwenye mipaka 31 iliyoko kwenye mikoa 14 yenye hatari ya kuingia kwa ugonjwa huu ambayo ni katika viwanja vya ndege vya: Julius Nyerere, Mwanza, Kilimanjaro, Bukoba, Songwe na Kigoma; bandari za Dar es Salaam, Tanga, Mwanza, Kasanga (Rukwa), Kigoma, Mbamba bay (Ruvuma) na Mtwara; mipaka ya nchi kavu ya Mtukula (Kagera), Murusagamba (Kagera), Mabamba (Kigoma), Kasesya (Rukwa), Manyovu (Kigoma), Ikola (Katavi), Kalambo (Mtwara), Rusumo (Kagera), Horohoro (Tanga), Kasumulo (Mbeya), Sirari (Mara), Murongo (Kagera), Tunduma( Songwe), Namanga (Arusha), Tarakea (Kilimanjaro), Kabanga (Kagera) na Mtambaswala (Mtwara).
Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto
25. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kuimarisha huduma za afya ya uzazi na mtoto ambapo, katika huduma kabla ya Ujauzito, Wizara kwa kushirikiana na wadau imenunua na kusambaza dawa mbalimbali kwa ajili ya uzazi wa mpango ili kuwezesha wanawake na wanaume kuamua lini, na ni watoto wangapi wanataka kuzaa na kwa kupishanisha muda gani. Katika kuimarisha huduma za afya wakati wa ujauzito (Antenatal Care), kwa kipindi cha Julai 2018 hadi Machi 2019, jumla ya wajawazito 1,264,767 walihudhuria kliniki wakati wa ujauzito, kati ya hao 892,936 walitimiza mahudhurio manne au zaidi (ANC4+) ambapo ni sawa na asilimia 70.6 ikilinganishwa na asilimia 48 kwa kipindi kama hicho mwaka 2017. Hadi kufikia mwezi Machi 2019 asilimia 28 ya wajawazito wote walihudhuria kliniki ndani ya wiki 12 ya tangu kuanza kwa ujauzito wao, asilimia 85.5 walihudhuria angalau mara moja na asilimia 69.4 walihudhuria angalau mara nne (4) ikinilinganishwa na asilimia 48.9 kwa kipindi kama hicho mwaka 2017. Nitumie fursa hii kuwahimiza wanawake wajawazito wote kuhudhuria kliniki Kama inavyoshauriwa na wataalam wa afya.
26. Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa huduma wakati wa Kujifungua, Wizara ilinunua dawa za uzazi salama na kuzisambaza kupitia Bohari Kuu ya Dawa (MSD). Upatikanaji wa dawa hizo umewezesha kupunguza vifo vya akinamama vitokanavyo na uzazi pingamizi. Aidha, dawa za watoto chini ya miaka mitano zilizonunuliwa na kusambazwa katika kipindi hiki. Upatikanaji wa dawa hizo umewezesha kuwatibu watoto waliopata magonjwa ya nimonia na kuharisha.
27. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kubuni mikakakti na kutafuta rasilimali fedha kwa ajili ya kuboresha vituo vya kutolea huduma za afya katika ngazi ya msingi ili viweze kutoa huduma bora ikiwa ni pamoja na huduma za uzazi wa dharura ikiwemo upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni (CEmONC). Katika kipindi cha mwaka 2018/19, Wizara kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI iliendelea kukamilisha ukarabati na ununuzi wa vifaa tiba katika vituo 352. Vituo hivyo, vimeendelea kuwezeshwa kutoa huduma za CEmONC pamoja na huduma zingine za upasuaji na hivyo kuongeza idadi ya akinamama wanaojifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya. Takwimu zinaonesha kuwa idadi ya akinamama wanaojifungulia katika vituo vya kutolea huduma imeendelea kuongezeka hadi kufikia asilimia 79.2 mwezi Machi 2019 ikilinganishwa na asilimia 68.5 mwezi Machi 2018. Napenda kutoa wito kwa wanawake wajawazito wote nchini, wajifungulie kwenye vituo vya kutolea huduma ya afya ili kupunguza vifo na changamoto za uzazi kwa mama na mtoto.
6
28. Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Wadau inatekeleza”Kampeni ya Jiongeze Tuwavushe Salama” yenye lengo la kuongeza kasi ya uwajibikaji katika ngazi zote ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga nchini. Katika kutekeleza Kampeni hiyo iliyozinduliwa na Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Novemba 2018, Wakuu wa Mikoa yote (26) ya Tanzania Bara walisaini Hati ya Makubaliano (MOU) na Mheshimiwa Makamu wa Rais na baada ya hapo Wakuu wa Mikoa walisaini Hati ya Makubaliano na Wakuu wa Wilaya ili kuhakikisha tunaongeza kasi na uwajibikaji katika kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi na watoto wa umri wa chini ya miaka 5 katika ngazi zote nchini. Tayari Mikoa yote imekwishazindua kampeni hii pamoja na kuandaa mpango kazi wa utekelezaji wa mikakati ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga kwa kila Mkoa na Wilaya zake. Aidha, Wizara imeongeza wigo wa ushauri wa kitaaluma toka kwa madaktari bingwa wabobezi wa nyanja zote kutoa ushauri wa kitaalamu kwenye vituo vya chini pindi wapatapo akinamama wenye matatizo magumu kuyatatua kwa njia ya "telemedicine" ya mtandao wa WhatsApp. Kupitia mfumo huu sekta ya afya imefanikiwa kunusuru maisha ya akinamama mijini na vijijini ambako madaktari bingwa wabobezi hawapatikani na kuongeza matumizi bora ya ufanisi kwa wataalam wetu wachache.
29. Mheshimiwa Spika, Katika kuimarisha huduma kwa mtoto na mtoto mchanga, Wizara imefanya mapitio ya miongozo mbalimbali ya mafunzo, kutengeneza na kukamilisha toleo la kwanza la mwongozo wa kitaifa wa huduma za mtoto mchanga na uanzishwaji wa vyumba maalum vya kuhudumia watoto wachanga (Neonatal Care Units). Aidha, jumla ya watoa huduma 2,320 toka Halmashauri 42 za Mikoa saba (7) ya Dodoma, Shinyanga, Simiyu, Kigoma, Tanga, Kagera na Mwanza wamepatiwa mafunzo juu ya Uthibiti wa Magonjwa ya watoto kwa uwiano “Integrated Management of Childhood Illness (IMCI). Vilevile, jumla ya wahudumu wa afya ngazi ya jamii 423 wamepewa mafunzo hayo pamoja na wasimamizi 22 juu ya huduma za Afya ya uzazi na mtoto ngazi ya jamii.
Huduma ya Lishe nchini
30. Mheshimiwa Spika, Lishe bora ni muhimu kwa uhai, ukuaji na maendeleo ya binadamu kiakili na kimwili na hivyo kuchangia katika kuongeza tija katika uzalishaji mali kwa kaya na kuimarisha uchumi wa Taifa kwa ujumla. Katika kuimarisha afya na lishe ya watoto wadogo, Wizara kwa kipindi cha mwezi Julai, 2018 ilitoa matone ya vitamini A kwa watoto 8,015,463 ambao ni sawa na asilimia 97.2 na mwezi Desemba 2018 imetoa matone ya vitamini A kwa watoto 8,305,565 ambao ni sawa na asilimia 97 ya watoto wote wa kati ya miezi 6 hadi miezi 59.
31. Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na wadau imeendelea kutoa virutubishi muhimu vya madini na vitamini kwa ukuaji wa mwili na akili wa wananchi kupitia urutubishaji wa unga wa ngano, unga wa mahindi na mafuta ya alizeti. Katika kipindi cha mwaka 2018/19 jumla ya mashine 62 za kusaga mahindi katika Mikoa ya Mbeya, Iringa, Shinyanga, Morogoro, Dodoma, Ruvuma, Tanga, Songwe, Njombe, Manyara na Dar Es Salaam zimefungwa kifaa maalum cha kuongeza virutubishi na hivyo kufanya idadi ya mashine zinazofanya urutubishaji kufikia 213 tangu utaratibu huu ulipoanzishwa nchini Mwezi Mei, 2013 zinazofanya urutubishaji huo.
Udhibiti wa UKIMWI
32. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea na mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI ambapo, Huduma za Ushauri Nasaha na Upimaji wa VVU zimeendelea kutolewa kwa wananchi wote bila malipo mijini na vijijini. Idadi ya watu waliopimwa VVU imeongezeka kutoka 10,577,881 mwaka 2017 hadi kufikia watu 14,368,114 Machi 2019
7
ambalo ni ongezeko la asilimia 35.8. Wizara kwa kushirikiana na wadau inatekeleza Kampeni, inayojulikana kama Furaha Yangu, Pima, Jitambue, Ishi inayolenga kuongeza idadi ya watu wanaopima VVU na kutambua hali zao ili kuanza dawa za ARV mapema. Napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) kwa kuzindua na kuwa balozi wa kampeni hii. Aidha ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote wakiongozwa na Mheshimiwa Job Ndugai - Spika waliojitokeza kupima VVU na kutambua hali zao. Aidha, Wizara kwa sasa ipo katika maandalizi ya mswada wa Marekebisho ya sheria ya VVU na UKIMWI (kuzuia na kudhibiti) Sura 431 ili kuruhusu watu kujipima VVU wenyewe na kushusha umri wa mtu kupima VVU bila ridhaa ya mzazi au mlezi kutoka miaka 18 hadi miaka 15.
33. Mheshimiwa Spika, Huduma za kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT), zimeendelea kutolewa, ambapo, jumla ya akina mama wajawazito 2,196,001 sawa na asilimia 97.2 ya akina mama 2,260,123 walipatiwa huduma za ushauri nasaha na upimaji wa VVU. Kati yao akina mama 78,238 sawa na asilimia 3.6 waligundulika kuwa wanaishi na VVU. Aidha, jumla ya Watoto 54,840 sawa na asilimia 70 walipata kipimo cha awali cha utambuzi wa maambukizi ya VVU ambapo watoto 1,865 sawa na asilimia 3.4 walikutwa na maambukizi. Kiwango hicho cha maambukizi kinaashiria Tanzania kufikia lengo la mwaka 2018 la kupunguza maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ya chini ya asilimia 4. Kwa mwenendo huu, Nchi ipo katika kasi sawia ya kuweza kufikia maambukizi chini ya asilimia 2 ifikapo mwaka 2021 kama inavyoainishwa katika mpango mkakati wa kutokomeza kabisa maambukizi ya VVU kwa watoto.
Udhibiti wa Kifua Kikuu na Ukoma
34. Mheshimiwa Spika, Wizara imefanikiwa kuongeza kasi ya ugunduzi wa wagonjwa wa Kifua Kikuu na kufikia lengo kwa asilimia 92 kwa kugundua wagonjwa 58,101 kwa kipindi cha Julai 2018 hadi Machi 2019 ikilinganishwa na wagonjwa 54,881 waliofikiwa mwaka 2017. Aidha, kiwango cha ugunduzi wa wagonjwa wa Kifua Kikuu kilipanda hadi kufikia asilimia 44 mwaka 2018 ikilinganishwa na asilimia 40 mwaka 2016. Katika kuimarisha huduma za upimaji wa TB, Wizara imeongeza mashine za kisasa za GeneXpert zinazopima kifua kikuu kwa ufanisi na muda mfupi kutoka 65 mwaka 2015 hadi 218 kwa sasa. Mashine hizi hutoa majibu ndani ya masaa 2 ikilinganishwa na hadubini ambazo hutoa majibu baada ya masaa 48. Hadi sasa jumla ya Halmashauri 111 kati ya 184 zimeshapatiwa mashine hizo. Halmashauri zilizobakia zinategemewa kupatiwa mashine hizi mwaka wa fedha 2019/20.
35. Mheshimiwa Spika, katika kuendelea na ugatuzi wa huduma za Kifua Kikuu Sugu, Wizara imefanikiwa kuongeza vituo vinavyotoa huduma hiyo kutoka vituo 61 mwezi Machi 2018 na kufikia 93 Machi 2019. Katika juhudi za kutanua wigo wa uibuaji wa wagonjwa wa Kifua kikuu, Wizara ilifanikiwa kuongeza maduka ya dawa muhimu yenye uwezo wa kuwaibua wahisiwa wa Kifua kikuu na kuwapatia rufaa kwenda kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa uchunguzi zaidi kutoka maduka 300 katika mikoa kumi mwaka 2017 hadi 450 katika mikoa kumi na tano Desemba 2018. Aidha, Wizara iliwajengea uwezo Waganga wa jadi wapatao 275 katika mikoa nane ya Simiyu, Kagera, Shinyanga, Dodoma, Ruvuma, Tanga, Mbeya na Mara ili kuweza kuchunguza Kifua Kikuu na kuwapa rufaa kwenda kwenye vituo vya afya.
36. Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa huduma za Ukoma; Kaya 82 zimetembelewa (contact tracing) na kufanya uchunguzi wa Ukoma katika wilaya za Muheza, Mkinga, Chato, Ifakara, Kilombero, Nanyumbu na Liwale. Zoezi hili limegundua wagonjwa wapya 46 na kuwaanzishia matibabu ya ukoma. Hadi kufikia Machi, 2019
8
wamegunduliwa wagonjwa 1,500 nchi nzima ukilinganisha na wagonjwa 1,835 kwa kipindi kama hiki cha mwaka 2017/2018.
Udhibiti wa Malaria
37. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kushirikiana na wadau katika kuhakikisha dawa za kutibu malaria na vitendanishi zinapatikana wakati wote katika vituo vya kutolea huduma za Afya. Wizara kupitia Bohari Kuu ya Dawa (MSD), imenunua vitendanishi vya malaria (mRDT) vipimo 29,878,375, Dawa Mseto ya malaria (ALu) dozi 9,381,360 kwa ajili ya matibabu ya malaria isiyo kali (uncomplicated malaria) na vidonge vya SP dozi 4,457,433 kwa ajili ya tiba kinga kwa wajawazito dhidi ya madhara yanayotokana na Malaria.
38. Mheshimiwa Spika, ili kuendelea kuwakinga wananchi wetu na maambukizi ya Malaria, Wizara imegawa jumla ya vyandarua 7,561,595 vyenye dawa bila malipo kwa jamii, kati ya hivyo, vyandarua 3,625,666 vilitolewa kwa wajawazito pamoja na watoto wenye umri wa miezi 9 walipohudhuria kwenye vituo vya kutolea huduma kwa ajili ya kupatiwa chanjo ya kwanza ya Surua-Rubella (MR1) na jumla ya vyandarua 2,757,969 viligawiwa kwa wanafunzi wa shule za msingi katika Halmashauri mbalimbali nchini. Napenda kuhimiza wananchi hasa wakinamama wajawazito na watoto wa umri wa chini ya miaka 5 kulala kwenye vyandarua vyenye dawa.
39. Mheshimiwa Spika, ili kuangamiza mbu wakiwa katika hatua ya viluwiluwi kwenye mazalia, Wizara katika kipindi cha mwaka 2018/19 imenunua viuadudu (biolarvicides) lita 60,000, Pampu za kunyunyizia zipatazo 1,000 na vifaa vingine muhimu ambavyo vinaendelea kusambazwa kwenye Halmashauri za Mikoa mitano (5) yenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya malaria ambayo ni Geita, Kagera, Kigoma, Lindi na Mtwara. Utekelezaji wa Afua hii, sio tu unadhibiti mbu wanaoeneza ugonjwa wa Malaria, bali pia magonjwa mengine ikiwa ni pamoja na homa ya Dengue, Zika, Matende, Homa ya manjano (Yellow fever), Chikungunya na Homa ya Bonde la Ufa.
40. Mheshimiwa Spika, Wizara imetekeleza zoezi la upuliziaji wa dawa-ukoko majumbani (Indoor Residual Spray) katika Halmashauri 7 za Mikoa minne yenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya malaria ambazo ni Ngara, Bukoba Vijijini, Misenyi, Chato, Nyang’hwale, Buchosa na Kakonko. Jumla ya nyumba zilizopuliziwa dawa ukoko katika kipindi cha Julai 2018 hadi Machi 2019 ni 501,587 ambayo ni sawa na asilimia 95.5 ya lengo kwa mwaka 2018, na kuweza kuwakinga jumla ya wananchi takribani 1,926,767 kutoka mikoa hiyo.
Udhibiti wa Magonjwa ya Mlipuko
41. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa hatari ya Mlipuko ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa Ebola. Kufuatia kuwepo kwa Ugonjwa wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambao ulianza Agosti 2018, Wizara imeandaa mpango mkakati wa nchi wa kukabiliana na tishio la ugonjwa huo. Watumishi 350 walipewa mafunzo kutoka mikoa iliyoko katika hatari zaidi ya kupata ugonjwa huu na iliyo mpakani na DRC na Uganda. Mikoa hiyo ni Kagera, Katavi, Rukwa, Songwe, Kigoma, Mbeya, Mwanza na Dar es Salaam. Aidha, Wizara imeendelea kutoa elimu kwa jamii kupitia njia mbalimbali na pia imeimarisha utambuaji wa ugonjwa wa Ebola kupitia Maabara ya Taifa, Maabara ya hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Mbeya na Maabara ya KCMC.
42. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kudhibiti ugonjwa wa Kipindupindu ambapo katika kipindi cha Julai 2018 hadi Machi 2019, jumla ya wagonjwa 2,050 wa Kipindupindu na vifo 28 vilitolewa taarifa nchini, ambapo mikoa 23 kati ya 26 iliweza kudhibiti ugonjwa huu kwa kiasi kikubwa. Hadi kufikia mwishoni wa mwezi Machi
9
2019, mikoa miwili ya Tanga na Arusha ndio pekee iliyokuwa inaendelea kutoa taarifa ya kuwepo kwa ugonjwa huu. Wizara yangu inakamilisha Mpango Mkakati wa kutokomeza kabisa Ugonjwa wa Kipindupindu ifikapo mwaka 2030. Mpango huu unategemewa kuanza kutumika mwaka 2019, na pia utajumuisha Sekta mbalimbali hususan za Maafa, Maji na Mazingira kwa sababu suala la kudhibiti kipindupindu ni suala mtambuka.
43. Mheshimiwa Spika, Wizara pia imeendelea kudhibiti ugonjwa wa Dengue ambao umekuwa ni tishio. Hadi kufikia Machi 2019, wagonjwa 523 wametolewa taarifa ambao kati yao, 467 wametokea Dar es salaam na 56 wametoka mkoa wa Tanga. Wizara imeshakamilisha mpango mkakati wa kudhibiti ugonjwa huu ambao unajumuisha kujenga uwezo wa watumishi wa afya katika kutambua, kupima, matibabu na udhibiti wa mbu wanaoeneza ugonjwa huu. Kupitia bunge lako tukufu, Ninatoa rai kwa wananchi kuwa makini wapatapo homa na wahakikishe wanakwenda kupata huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya ili waweze kupimwa na kupatiwa tiba sahihi.
Udhibiti wa Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele
44. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2018 hadi Machi 2019, Wizara iliratibu zoezi la utoaji wa dawa za Kingatiba kwa magonjwa ya Minyoo ya Tumbo na Kichocho kwa Watoto wenye umri wa kwenda shule ya Msingi wapatao 5,755,447 kutoka Halmashauri 91 nchini, ikilinganishwa na watoto 7,917,080 waliofikiwa mwaka 2017/18. Kwa ugonjwa wa Trachoma, watu waliopatiwa kingatiba walifikia 1,345,426 kutoka Halmashauri 6 kati ya 8 zilizolengwa kupatiwa kingatiba hiyo ikilinganishwa na watu 2,310,012 kutoka Halmashauri kumi na moja (11) kwa mwaka 2017/18. Takwimu hizi zinaonesha kuwa kuna punguzo la maambukizi ya ugonjwa wa trachoma kwenye halmashauri 3 kutoka halmashauri 11 za mwaka 2017/18 ambazo ni Bahi, Nkasi na Ngara. Aidha, kwa ugonjwa wa Usubi watu 4,197,915 kutoka Halmashauri 26 nchini walipatiwa kingatiba ya usubi kwa mwaka 2018/2019 ikilinganishwa na watu 4,446,015 kutoka Halmashauri 28 kwa mwaka 2017/18. Halmashauri 2 za Mkinga na Muheza bado zinaendelea na zoezi hili. Kwa ugonjwa wa Matende na Mabusha, watu wapatao 8,175,280 walipatiwa kingatiba ya matende na mabusha kwa mwaka 2018/19 katika Halmashauri 24, ikilinganishwa na watu 8,517,580 kutoka Halmashauri 27 kwa mwaka wa fedha 2017/18. Hivyo halmashauri 3 za Chemba, Kondoa na Kondoa Mji zimedhibiti ugonjwa huo katika kipindi cha mwaka huu wa 2018/19.
Elimu ya Afya kwa Umma
45. Mheshimiwa Spika, Wizara iliendelea kutoa elimu kwa jamii katika masuala mbalimbali ikiwemo lishe, kujikinga na magonjwa ya kuambukiza, magonjwa yasiyo ya kuambukiza na yale ambayo hayapewi kipaumbele. Aidha, Wizara imefanya uhamasishaji wa wananchi katika kupima VVU, kupima saratani, kupima TB, kuchangia damu, kupima afya zao na kufanya mazoezi mara kwa mara ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza, pamoja na kuwajengea uwezo timu za Mikoa na Halmashauri ili kuelewa majukumu yao. Wizara imeandaa mfumo wa upashanaji taarifa za afya kupitia jukwaa la uhamasishaji la kielektroniki (Health Promotion Digital Platform) ambapo mteja anaweza kupiga namba *152*05# na kupata taarifa za uelimishaji na uhamasishaji huduma za afya.
HUDUMA ZA TIBA
Usimamizi wa Vituo vya kutolea huduma za Afya
46. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia upatikanaji wa huduma za afya nchini zinazitolewa kupitia vituo vya kutolea huduma vya Serikali, binafsi na mashirika ya dini. Katika kipindi cha Julai 2018 hadi Machi 2019, vituo vya kutolea
10
huduma za afya nchini vimeongezeka kufikia 8,119 ikilinganishwa na vituo 7,678 mwezi Juni 2018 kama ilivyoainishwa katika Hotuba.
Upatikanaji wa Dawa, Vifaa na Vifaa Tiba na Vitendanishi
47. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa Dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi kwa kuiwezesha Bohari ya Dawa (MSD) kununua, kutunza na kusambaza dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vya umma. Hadi kufikia mwezi Machi 2019 upatikanaji wa dawa muhimu aina 30 kwenye Vituo vya kutolea huduma za afya umefikia asilimia 94.4 Mchanganuo wa upatikanaji wa dawa hizi kimkoa ni kama ilivyoainishwa. Aidha, katika kuboresha huduma za uchunguzi wa magonjwa, Wizara imenunua Mashine za X-ray 11 za Kidigitali na kupelekwa katika hospitali za rufaa za mikoa ya Ruvuma, Morogoro, Simiyu, Singida, Njombe, Kagera, Amana (DSM), Katavi na Hospitali za wilaya za Magu, Chato na Nzega. Vilevile, Wizara ilinunua na kusambaza vifaa na vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi bilioni 97.3 katika vituo vya Afya 318 vilivyojengwa na kukarabatiwa katika Halmashauri mbalimbali nchini ili viweze kutoa huduma bora za Afya ikiwemo upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni.
48. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuimarisha huduma za kibingwa za magonjwa ya Kinywa na meno kwa kununua Viti vya Huduma ya Kinywa yaani (Dental Chair) 20 na Mashine za Mionzi za Huduma ya Kinywa (Dental X-ray) 8 ambazo zinafungwa katika hospitali za Rufaa za Mikoa na hospitali za Halmashauri. Aidha, Wizara imeanza mchakato wa kununua Vifaa, Vifaa Tiba na Vitendanishi kwa mfumo wa Kukodi vifaa vya maabara na vitendanishi yaani (Reagent Rental System) ili kuipunguzia mzigo Serikali wa kununua na kusambaza vifaa hivi katika vituo vya kutolea huduma vya umma. Faida za Mfumo huu wa MES ni pamoja Kupata vifaa vyenye teknolojia ya kisasa, Kuepusha gharama za kuharibu vifaa vinavyomaliza muda wake wa matumizi na Kuondoa gharama kubwa za matengenezo ya Vifaa, Mashine na Vifaa Tiba.
49. Mheshimiwa Spika, Vilevile Wizara imenunua jumla ya Digital X-rays 28 na LED Microscope 389 kupitia fedha za Mfuko wa Kupambana na VVU, Malaria na Kifua Kikuu (Global Fund). Vifaa hivyo vinasambazwa katika mikoa ya Iringa, Kilimanjaro, Mara, Mbeya, Ruvuma, Tanga, Rukwa, Njombe, Songwe na Dar es Salaam.
50. Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Wizara ya Viwanda na Biashara na Uwekezaji, Kituo cha Uwekezaji (Tanzania Investment Center -TIC) na Bohari ya Dawa imeandaa mwongozo unaoainisha fursa mbalimbali za Uwekezaji katika Viwanda vya dawa na vifaa tiba nchini (Guidelines for Investment Opportunities in Pharmaceutical Industries) 2018. Mwongozo huo utarahisisha upatikanaji wa taarifa katika uwekezaji wa viwanda vya dawa nchini. Hadi kufikia Machi, 2019 viwanda nane (8) vya dawa vinaendelea kujengwa nchini. Viwanda hivyo ni Kairuki Pharmaceuticals, Biotech Laboratories, Vista Pharma, Afravet/ Novel Vaccines and Biological, Hester Biosciences Africa, Afrikana Pharmaceuticals, Alfa Pharmaceuticals na Pharm Access. Sambamba na hilo Wizara imefuta tozo 14 na kupunguza tozo zingine 17 zilizokuwa zinatozwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) pamoja na Mkemia Mkuu wa Serikali ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha inaweka mazingira wezeshi ya kibiashara na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kuvutia uzalishaji wa ndani wa dawa.
Upatikanaji wa Damu Salama
51. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Mpango wa Taifa wa Damu Salama ilipanga kukusanya chupa za Damu Salama 375,000 ili kukidhi mahitaji ya damu salama nchini katika kipindi cha mwaka mzima wa 2018/2019. Hadi kufikia Machi, 2019 jumla ya
11
chupa za damu salama 235,381 zilikusanywa, sawa na asilimia 63 ya lengo la mwaka ikilinganishwa na chupa 119,753 zilizokusanywa katika kipindi cha mwaka 2017.
Uimarishaji wa huduma za Matibabu ya Kibingwa nchini
52. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuboresha na kuimarisha huduma za matibabu ya kibingwa nchini, ili kuokoa maisha ya wananchi wengi sambamba na kupunguza idadi ya wagonjwa wanaopewa rufaa ya Matibabu nje ya nchi. Katika kipindi cha Julai 2018 hadi Machi 2019 Hospitali za Rufaa za Kanda na Taifa ziliwasilisha Wizarani idadi ya wagonjwa 62 waliokuwa na mahitaji ya kupatiwa matibabu nje ya nchi, ikilinganishwa na wagonjwa 114 katika kipindi Julai 2017 hadi Machi 2018. Magonjwa yaliyoongoza ni pamoja na saratani wagonjwa (16), moyo (15), mifupa (12), mishipa ya fahamu (6), mishipa ya damu (5), figo (1) na magonjwa mengine (7).
53. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuimarisha huduma za kibingwa za kibobezi zinazotolewa katika hospitali ya Taifa na hospitali Maalum. Katika kufanikisha hilo Serikali imeendelea kuimarisha ushirikiano kati yake na nchi mbalimbali ikiwemo China katika eneo la Afya. Mnamo mwezi Agosti 2018, timu ya viongozi na wataalam wa Wizara ya Afya walifanya ziara nchini China ikiwa ni kutekeleza makubaliano yaliyoingiwa na Viongozi Wakuu wa nchi hizi mbili. Makubaliano hayo yalilenga katika ushirikiano wa Tiba bobezi (Specilized medical services), kubadilishana wataalam, kufanya Tafiti kwa pamoja katika eneo la afya na kutoa mafunzo katika eneo la tiba bobezi kupitia Taasisi ya Saratani Ocean Road, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete na Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI).
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)
54. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2018 hadi Machi 2019, Hospitali ya Taifa Muhimbili imeona jumla ya wagonjwa 419,931. Lengo likiwa ni kuhudumia wagonjwa 300,000. Ongezeko la wagonjwa limetokana na kuboresha miundombinu na kuongeza upatikanaji wa huduma mbalimbali. Aidha, mambo makubwa yaliyotekelezwa na Hospitali ya Muhimbili katika kipindi hiki yameainishwa. Kwa umuhimu naomba niyatambue machache ambayo ni
(i) Hospitali ilitoa huduma za mikoba (outreach medical services) katika mikoa ya Mara, Lindi na Mtwara ambapo zaidi ya wagonjwa 4,700 katika mikoa hiyo walipata huduma.
(ii) Jumla ya wagonjwa 29 walipata huduma ya upandikizwaji wa figo (Renal transplant) na kufikisha jumla ya wagonjwa 38 waliopata huduma hii toka Hospitali ilipoanza kutoa huduma za kupandikiza figo mwezi Novemba 2017.
(iii) hospitali imetoa huduma za kupandikiza vifaa vya usikivu kwa watoto (cochlear implant) 11 na kufikisha jumla ya watoto 21 waliopata huduma hii toka ilipoanza mwezi Juni, 2017
Hospitali ya Mloganzila
55. Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha Julai 2018 hadi Machi 2019 Hospitali imehudumia jumla ya wagonjwa 40,639. Katika kuimarisha usimamizi wa Hospitali hii na kufuatia maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 3 Oktoba 2018, uendeshaji wa hospitali ulikabidhiwa kwa Bodi na Menejimenti ya Hospitali ya Taifa Muhimbili kutoka Chuo Kikuu cha Afya cha Muhimbili. Baada ya makabidhiano, Hospitali ya Taifa Muhimbili ilifanya mapitio ya mfumo wa uendeshaji na kufunga mifumo ya TEHAMA na kuimarisha upatikanaji wa huduma ikiwemo uanzishwaji wa usafiri wa mabasi (daladala) kufika
12
Hospitalini. Hatua hii imewezesha kupunguza kero na malalamiko mbalimbali yaliyokuwa yakitolewa na wananchi kuhusu hospitali ya Mloganzila.
Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI)
56. Mheshimiwa Spika, Taasisi ya Mifupa (MOI) imeendelea kutekeleza majukumu yake ya kutoa huduma ya matibabu ya mifupa, upasuaji mishipa ya fahamu na ubongo ambapo jumla ya wagonjwa 221,801 walipatiwa matibabu. Mambo makubwa yaliyotekelezwa na MOI yameainishwa na baadhi ya maeneo hayo ni pamoja na
(i) Hospitali ilifanya upasuaji bobezi kwa wagonjwa 4,885 kati yao wakiwemo; upasuaji mifupa, kubadilisha nyonga, goti, upasuaji wa goti kwa kutumia matundu, upasuaji wa mfupa wa kiuno, upasuaji wa uti wa mgongo, ubongo, watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi, na wagonjwa wa dharura na kuokoa zaidi ya shilingi bilioni 10 kama wangepewa rufaa nje ya nchi.
(ii) Kukamilisha vyumba vitatu (3) vipya vya upasuaji na kufanya vyumba vya upasuaji kuwa 9 mwaka 2018/2019 kutoka vyumba 6 mwaka 2017/2018, hivyo kuongeza idadi ya wagonjwa wanao wafanyiwa upasuaji kufikia 700 hadi 900 kwa mwezi mwaka 2018/2019 tofauti na 400 hadi 600 kwa mwezi mwaka 2017/2018
(iii) Kufanya kwa mara ya kwanza upasuaji wa vivimbe vya damu kwenye ubongo (cerebral aneurysm) baada ya kununua kifaa cha kisasa cha kufanyia upasuaji wa mishipa ya fahamu na ubongo (Neurosurgeries), vibanio maalum (clips) na seti maalum ya vifaa vya upasuaji huu pamoja na mashine maalum ya kufungulia fuvu (High power drill) vyenye thamani ya shilingi milioni 150.
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
57. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2018 hadi Machi, 2019, Taasisi ilihudumia wagonjwa wa nje 69,601 na wagonjwa wa ndani 2,825. Mafanikio makubwa yaliyopatikana ni pamoja na;
(i) Taasisi imeweza kufanya upasuaji kwa wagonjwa 330 wenye matatizo ya mishipa ya damu.
(ii) wagonjwa 964 walipatiwa matibabu ya moyo kupitia mtambo maalum “Catheterization Laboratory”
(iii) Kukamilisha ukarabati wa jengo la wodi mpya ya watoto ambayo inalenga kutoa huduma bora kwa watoto wenye matatizo ya moyo.
Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI)
58. Mheshimiwa Spika, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road imeendelea kutoa huduma kwa wagonjwa wa Saratani ambapo katika kipindi cha Julai, 2018 hadi Machi, 2019 jumla ya wagonjwa 53,324 walihudumiwa. Mafanikio makubwa yaliyofikiwa na Hospitali yameainishwa ukurasa wa 62 hadi 65 wa hotuba yangu. Kwa umuhimu naomba niyatambue yafuatayo;
(i) Jumla ya wananchi 10,564 walifanyiwa Uchunguzi uliofanywa ulihusisha upimaji wa saratani za mlango wa kizazi, matiti, tezi dume, saratani ya ngozi (Kaposi sarcoma) na saratani ya ngozi kwa wenye ualbino katika mikoa ya Dar-es-Salaam Pwani, Tabora, Singida, Lindi na Dodoma.
(ii) Jumla ya tiba 51,327 za mionzi ya nje na 1,563 za mionzi ya ndani zilitolewa kwa wagonjwa katika Taasisi kwa kutumia mashine 5 za mionzi ya nje (2 - Cobalt 60, 1 - caesium, 2 - LINAC) na mashine 2 mionzi ya
13
ndani (brachytherapy) zilizonunuliwa na Serikali kwa fedha za ndani Shilingi bilioni 9.5
(iii) Hospitali imeweza kupunguza muda wa kusubiri kuanza tiba za mionzi kwa wagonjwa kuwa chini ya wiki 4 kutoka wiki 6; Hapo awali muda wa kusubiri tiba mionzi ulikuwa wiki 12 (mwaka 2015
Sambamba na jitihada za Serikali za kuimarisha huduma za matibabu ya Saratani nchini, ninapenda kutumia Bunge lako Tukufu kuhimiza wananchi kupima Saratani angalau mara moja kwa mwaka ili endapo wanadalili za saratani waweze kupata matibabu haraka kwani saratani inatibika ikigundulika mapema.
Hospitali ya Benjamin Mkapa-Dodoma
59. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Hospitali imeendelea kutoa huduma ambapo jumla ya wagonjwa 65,223 walihudhuria na kupata matibabu. Kati ya hao, wagonjwa 64,889 walikuwa wa nje (OPD) na wagonjwa waliolazwa (IPD) 3,334. Mafanikio yaliyopatikana Benjamin Mkapa ni pamoja na
(i) upandikizaji figo ulifanywa kwa wagonjwa 7 tangu huduma hiyo kuanzishwa.
(ii) huduma ya uchunguzi na matibabu ya moyo kwa kutumia maabara maalumu “cathlab” yenye thamani ya shilingi 2,449,648,100 zilianzishwa na jumla ya wagonjwa 12 wamenufaika na huduma hizi toka ilipozinduliwa Februari, 2019
Hospitali ya Afya ya Akili Mirembe
60. Mheshimiwa Spika, Katika kuimarisha utoaji wa huduma maalum, Hospitali ya Afya ya Akili Mirembe na Taasisi ya Isanga imeendelea kutoa huduma kwa wagonjwa wa afya ya akili. Katika mwaka 2018/19 jumla ya Wagonjwa 181,981 walipatiwa huduma. Hali ya upatikanaji wa dawa za wagonjwa wa akili imeimarishwa na kufikia asilimia 100.
Hospitali ya Rufaa ya Magonjwa ya Kifua Kikuu (Kibong'oto)
61. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, hospitali iliendelea kutoa huduma za utambuzi na matibabu ya Kifua Kikuu, Kifua kikuu sugu, VVU na magonjwa mengine ya kuambukiza. Jumla ya wagonjwa 18,888 walipatiwa huduma
Hospitali ya Rufaa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya)
62. Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Rufaa ya Kanda za Nyanda za Juu Kusini imeendelea kutoa huduma za matibabu ya kibingwa hususan kwa wananchi wa mikoa 6 ya Katavi, Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa ambapo katika kipindi cha Julai 2018 hadi Machi 2019, hospitali imehudumia jumla ya wagonjwa 234,360. Hali ya upatikanaji wa dawa imeendelea kuimarishwa na kufikia asilimia 95. Hospitali pia imenunua “CT Scan” yenye thamani shilingi 1,170,590,000 ambayo ipo katika hatua ya ufungwaji na huduma zinategemewa kuanza kutolewa mwezi Mei 2019.
Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa (Bugando)
63. Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa,
64. Bugando imeendela kutoa huduma za kibingwa kwa wagonjwa kutoka mikoa 6 ya Mwanza, Geita, Simiyu, Shinyanga, Kagera, Mara na Kigoma. Katika kipindi cha Julai, 2018 hadi Machi, 2019, ilihudumia jumla ya Wagonjwa 250,721 ikilinganishwa na wagonjwa 180,521 katika kipindi kama hicho mwaka 2018. Hospitali ya Bugando imeendelea kupanua huduma za kibingwa kwa kuanza kutoa matibabu yote ya Saratani baada ya kununua mashine ya tiba ya mionzi iitwayo Brachytherapy kwa Shilingi 1,400,000,000. Upatikanaji wa huduma hii umepunguza rufaa za wagonjwa wa saratani wa kanda ya ziwa kwenda Taasisi ya Saratani Ocean Road kwa zaidi ya asilimia 95.
14
Hospitali ya Rufaa ya Kanda Kaskazini (KCMC)
65. Mheshimiwa Spika, Hospitali imeendelea kuboresha na kutoa huduma kwa wananchi ambapo katika kipindi cha Julai 2018 hadi Machi 2019, jumla ya wagonjwa 120,177 walipatiwa huduma za afya. Asilimia 79.7 ya wagonjwa wote waliohudumiwa walitoka kwenye mikoa mitano inayohudumiwa na hospitali ambayo ni Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Tanga na Singida, na asilimia 20.3 ya wagonjwa walitoka katika mikoa mingine ya Tanzania.
Hospitali za Rufaa za Mikoa
66. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha utoaji wa huduma katika Hospitali za Rufaa za Mikoa, usimamizi na uendeshaji wa hospitali hizo ulikabidhiwa Wizara ya Afya kutoka OR-TAMISEMI kuanzia Julai 2018 na hii ni kufuatia agizo la Mheshimiwa Dkt John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania alilolitoa Novemba 2017 . Kwa kipindi cha Julai 2018 hadi Machi 2019, Hospitali 28 za Rufaa za Mikoa zilihudumia jumla ya wagonjwa 3,292,103 kama inavyoonesha kwenye jedwali namba 2 la hotuba yangu.
67. Mheshimiwa Spika, katika kuboresha huduma za uchunguzi wa magonjwa, Wizara imenunua Mashine za X-ray 8 za Kidigitali na kupelekwa katika hospitali za rufaa za mikoa ya Ruvuma, Morogoro, Simiyu, Singida, Njombe, Kagera, Amana (DSM) na Katavi. Aidha, katika kuboresha utoaji wa huduma kwenye hospitali za Rufaa za Mikoa, Wizara imeweka kipaumbele katika kuboresha/kujenga miundombinu ya huduma za dharura (EMD), huduma za uzazi na mtoto (Maternity Block) na huduma ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU).
68. Mheshimiwa Spika, ujenzi wa majengo ya kutolea huduma za uzazi unaendelea katika hospitali za rufaa za Sekou Toure (Mwanza), Mwananyamala (DSM), Simiyu, Mawenzi (Kilimanjaro), Shinyanga na Njombe. Aidha, majengo ya kutolea huduma za dharura yanaendelea kujengwa katika hospitali za Sokoine (Lindi), Mwananyamala, Amana, Temeke (DSM) na hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera. Mchakato wa kuanza ujenzi wa jengo la upasuaji katika hospitali ya Mkoa wa Kigoma (Maweni) umeanza. Vilevile, Wizara imeanza ujenzi wa wodi za kulaza wagonjwa katika hospitali za Mikoa ya Pwani na Mbeya. Kama ilivyoelekezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/20 Serikali imeanza ujenzi wa Hospitali za rufaa za mikoa katika mikoa mipya ya Songwe, Katavi, Njombe, Geita na Simiyu ambapo ujenzi upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na Serikali imeshatoa jumla ya shilingi bilioni 6.5 kwa ajili ya ujenzi huo.
UHAKIKI UBORA WA HUDUMA ZA AFYA 69. Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha huduma za afya nchini ambapo Mfuko wa Dunia (Global Fund) tayari wameidhinisha bajeti ya Shilingi 23,646,951,900 ili kuboresha vituo vya kutolea huduma za afya katika ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa pamoja na ngazi ya Hospitali za Rufaa za Mikoa. Mgawanyo wa fedha hizo ni Shilingi 10,928,729,500 zitapelekwa katika Hospitali za Rufaa za Mikoa zinazofanyiwa maboresho katika Huduma za Wazazi, Shilingi 3,119,302,400 zitapelekwa katika Hospitali za Rufaa za Mikoa zinazofanyiwa maboresho katika Huduma za Dharura, Shilingi 3,000,000,000 zilizotengewa kwa ajili ya Zahanati, Shilingi 1,200,000,000 kwa ajili ya vituo vya Afya, Shilingi 3,600,000,000 kwa ajili ya hospitali za wilaya na Shilingi 1,798,920,000 kwa ajili matibabu ya Kifua Kikuu sugu katika Vituo vya Afya.
UGHARAMIAJI WA HUDUMA ZA AFYA
70. Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na maandalizi ya kukamilisha Muswada wa kutunga sheria ya bima ya afya kwa watu wote. Mswada huu unatarajiwa
15
kuwasilishwa bungeni mwezi Septemba, 2019. Aidha, Mkutano wa kuelimisha waheshimiwa wabunge kuhusu mkakati wa Ugharamiaji wa Huduma za Afya pamoja na mkakati wa kuboresha mfumo wa Bima ya Afya ya Taifa ulifanyika mwezi Januari 2019. Vilevile, Wizara ilifanikisha ziara ya Waheshimiwa wabunge 19 nchini Rwanda na Ghana mwezi Desemba 2018 lengo likiwa ni kupata uzoefu wa namna nchi mbalimbali zilivyoweza kutekeleza mfumo wa Bima moja kwa watu wote.
RASILIMALI WATU KATIKA SEKTA YA AFYA
71. Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka 2018/19 jumla ya wanafunzi 18,539 walidahiliwa na vyuo vya afya kwa ajili ya kusoma kozi mbalimbali za afya kada za kati. Idadi hiyo ni sawa na asilimia 123.59 ya lengo kudahili Wanafunzi 15,000 kwa mwaka ifikapo 2020 kama ilivyoelekezwa kwenye Ilani ya Uchanguzi ya Chama Tawala (CCM). Kwa upande wa watoa huduma, jumla ya vibali vya ajira kwa watumishi 8,071 vilitolewa katika kipindi hiki ambapo watumishi wa afya 6,180 walipelekwa OR-TAMISEMI na watumishi 1,891 walipelekwa Hospitali zilizo chini ya Wizara ya Afya. Aidha, kwa mwaka 2019/20 Wizara imewasilisha maombi ya ajira mpya kwa Sekta ya Afya yenye jumla ya nafasi 12,775. Ni matarajio ya Wizara kuwa kibali hicho kitatolewa kabla ya mwaka wa fedha kuisha. Vilevile, jumla ya nyumba za watumishi 318 zimejengwa kwa lengo la kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa Sekta ya Afya. Nitumie fursa hii kuzitaka halmashauri zote nchini hasa za pembezoni kuweka mazingira mazuri na vivutio kwa watumishi wa afya kufanya kazi katika halmashauri zao. Aidha, natoa rai kwa viongozi wa mikoa, wilaya na halmashauri kuzingatia sheria, taratibu na kanuni katika kushughulikia nidhamu na uwajibikaji wa wataalam wa afya katika maeneo yao.
D. UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA TAASISI CHINI YA IDARA KUU YA AFYA (FUNGU 52)
Utekelezaji wa majukumu ya Taasisi zilizo chini ya Fungu 52 umeainishwa kuanzia ukurasa wa 95 hadi 113 wa hotuba yangu.
Bohari ya Dawa (MSD)
72. Mheshimiwa Spika, Tathimini ya upatikanaji wa aina 312 za dawa, vifaa na vifaa tiba hadi kufikia Machi 2019 ilikuwa ni asilimia 79. Hali hii imetokana na juhudi za Bohari ya Dawa kuingia mikataba ya moja kwa moja na wazalishaji wa dawa ambapo mpaka mwishoni mwa mwezi Machi, 2019, Bohari ya Dawa ilikuwa imeingia mikataba ya muda mrefu (Framework Agreement) na jumla ya wazalishaji 128, kati yao 17 wakiwa ni wazalishaji wa ndani. Hatua hii inakusudiwa kuhakikisha upatikanaji wa aina zote 680 za dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi unaendelea kuimarika na kwa wakati katika maghala yote ya Bohari ya Dawa (MSD) kulingana na upatikanaji wa fedha. 73. Mheshimiwa Spika, Bohari ya Dawa pia imekamilisha maandalizi ya ununuzi wa dawa za nchi 16 za Jumuia ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kupitia mfumo wa Pooled Procurement Services (PPS). Mfumo huu utasaidia kupunguza gharama za ununuzi wa dawa nchini kutokana na kupata mahitaji (orders) kwa bei nafuu.
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF)
74. Mheshimiwa Spika, Mfuko uliweze kuandikisha Wanachama wapya wachangiaji 275,247 ikilinganishwa na idadi ya wanachama 167,791 mwaka 2017/18. Ongezeko hili limewezesha Mfuko kuwa na jumla ya wanufaika 4,217,211 sawa na asilimia 8 ya wananchi wote nchini. Kwa upande wa Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF), kaya 2,171,606 zenye jumla ya wanafuika 13,029,636 zimeandikishwa katika halmashauri mbalimbali nchini. Hadi kufikia Machi 2019, idadi ya wananchi wanaopata matibabu kupitia Mifuko ya Bima ya Umma ni 17,246,847 sawa na asilimia 33 (asilimia 8 NHIF na asilimia 25 CHF) ya wananchi wote. Kupitia Mradi wa Tumaini la mama
16
unaotekelezwa katika Mikoa ya Tanga, Mbeya, Lindi, Mtwara na Tanga kwa lengo la kupunguza vifo vya wanawake vitokanavyo na uzazi, Mfuko umesajili wanufaika wapya 166,941. Hivyo, jumla ya kina mama 1,157,191 wamenufaika tangu kuanzishwa kwake mwaka 2012.
75. Mheshimiwa Spika, Katika kipindi hicho Mfuko ulikusanya kiasi cha shilingi bilioni 261.52 ikiwa ni michango kutoka kwa wanachama wake. Aidha, Mfuko ulilipa watoa huduma jumla ya shilingi bilioni 218.01 ambapo kati ya hizo asilimia 36 zililipwa kwa vituo vya Serikali, asilimia 35 kwa vituo Binafsi na asilimia 29 kwa vituo vya Madhehebu ya Dini. Aidha kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2014/15 hadi 2017/18 malipo kwa watoa huduma hasa wa Serikali yameongezeka kwa wastani wa asilimia 146 kutoka shilingi bilioni 44.87 hadi shilingi bilioni 133.98. Hivyo napenda natoa maelekezo kwa watoa huduma wote wa Serikali, kutumia fedha hizi za bima afya kuongeza mapato ya vituo na kuendelea kuboresha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi. Aidha, ninavitaka vituo vya umma kuboresha huduma zao ili kuvutia wananchi wengi hasa walio na Bima kupata huduma za afya katika vituo hivi.
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA)
76. Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ilifanya tathmini ya maombi 1,750 kati ya maombi 1,949 ya usajili wa vyakula yaliyopokelewa. Maombi 1,015 yaliyofanyiwa tathmini yaliidhinishwa. Aidha, maombi 69 yalikataliwa kwa kutokidhi vigezo na 666 yalikuwa na hoja. Mamlaka ilifanyiwa tathmini na Shirika la Afya Duniani (WHO) ambapo matokeo ya tathmini hiyo yameonyesha kuwa TFDA ina mifumo thabiti ya udhibiti wa dawa. Kutokana na matokeo hayo, Mamlaka ilitunukiwa cheti ya ngazi ya tatu ya umahili kitaalam (Maturity level 3) mwezi Novemba 2018, ngazi hii ni ya juu sana na hivyo kuifanya TFDA kuwa Mamlaka ya kwanza Barani Afrika kufikia hatua hiyo.
Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC)
77. Mheshimiwa Spika, ili kuimarisha huduma za lishe kwa wanawake na watoto wachanga kwenye ngazi ya jamii Taasisi imeendelea kutoa mafunzo ya matumizi ya Mkoba wa Siku 1000 (nyenzo ya kuhamasisha mabadiliko ya tabia kwenye jamii kupitia vikundi shirikishi) kwa watoa huduma za afya na lishe katika ngazi za jamii 468 katika mikoa ya Mtwara (Newala na Tandahimba), Mwanza (Ukerewe), Geita (Chato, na Mbogwe), Mara (Butiama), Kagera (Misenyi na Biharamlo), Kigoma (Buhigwe na Kasulu), Arusha na Manyara.
Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA)
78. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2018 hadi Machi 2019, Mamlaka imetekeleza yafuatayo:- jumla ya sampuli 59,693 zinazojumuisha makosa ya jinai, vinasaba, maji, maji taka, kemikali, vyakula, dawa na bidhaa nyingine za viwandani zilipokelewa kwa ajili ya uchunguzi. Sampuli zilizochunguzwa ni 44,173 sawa na asilimia 74.
Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR)
79. Mheshimiwa Spika, Miradi inayoendelea kutekelezwa na Taasisi hii katika maeneo mbalimbali nchini imeorodheshwa katika ukurasa 107 hadi 113 wa hotuba yangu. Miradi hiyo inalenga kutoa majibu na takwimu katika magonjwa ya Malaria, Virusi vya UKIMWI (VVU), Kifua kikuu na Magonjwa ya kitropikia yaliyokuwa hayapewi kipaumbele na Saratani ya shingo ya uzazi.
E. UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU CHINI YA IDARA KUU YA MAENDELEO YA JAMII (FUNGU 53)
17
Utekelezaji wa majukumu ya Fungu 53 umeainishwa kuanzia ukurasa wa 113 hadi 150 wa hotuba yangu.
80. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, utekelezaji wa majukumu ya Wizara (Fungu 53) ulijikita katika maeneo yafuatayo:
Kuamsha Ari ya Wananchi Kushiriki katika Shughuli za Kuleta Maendeleo
81. Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo ili kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kutumia nguvu kazi pamoja na rasilimali zinazowazunguka katika maeneo yao. Miradi hiyo ni: ujenzi wa skimu ya umwagiliaji katika Wilaya ya Mvomero (Wami, Lulindo na Dakawa) Mkoa wa Morogoro; ujenzi wa Shule Shikizi katika Wilaya ya Kibiti Mkoa wa Pwani kwa ajili ya watoto wadogo wasioweza kutembea umbali mrefu wa zaidi ya kilometa 5 kufuata shule ilipo; ujenzi wa bweni la wasichana katika Shule ya Sekondari Kirare Tanga Jiji (Tanga); ujenzi wa bweni katika Shule ya Sekondari ya Mikaranga mkoa wa Ruvuma; ujenzi wa zahanati katika Kijiji cha Mhagawa Asili, Wilayani Mbinga katika Mkoa wa Ruvuma pamoja na ujenzi wa wodi ya mama na mtoto kwenye Kituo cha Afya Kaloleni Arusha Jiji mkoani Arusha.
Mafunzo ya Taaluma ya Maendeleo ya Jamii
82. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia utoaji wa mafunzo kwa kada ya Maendeleo ya Jamii kupitia vyuo nane vya Maendeleo ya Jamii vya; Buhare, Uyole, Rungemba, Mlale, Misungwi, Ruaha, Mabughai na Monduli. Katika mwaka 2018/19, jumla ya wanafunzi 3,414 walidahiliwa ikilinganishwa na wanafunzi 2,677 waliodahiliwa mwaka 2017/18.
Kuimarisha Upatikanaji wa Haki za Mtoto
83. Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na wadau imeendelea kuhakikisha uwepo wa haki za mtoto za kuishi, kuendelezwa, kushiriki, kulindwa na kutobaguliwa katika jamii. Mwezi Desemba, 2018, Wizara kwa kushirikiana na wadau iliwezesha kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa Baraza la Watoto la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, hadi Machi, 2019, ushiriki wa watoto katika ajenda ya maendeleo unafanyika kupitia mabaraza ya watoto 1,669 yaliyopo katika ngazi ya Taifa, Mikoa, Halmashauri, Kata na Vijiji/Vitongoji na klabu za watoto 2,475 zilizoanzishwa katika shule za msingi na sekondari.
84. Mheshimiwa Spika, Huduma ya Simu kwa Watoto Na.116 imewezesha jumla ya mashauri 43 ya watoto kupewa rufaa kwa Maafisa Ustawi wa Jamii na Dawati la Jinsia na Watoto kwenye Vituo vya Polisi. Mashauri hayo yalihusu kutelekeza watoto (15), ubakaji (19), kudhuru mwili (2), ndoa za utotoni (2) na usafirishaji haramu wa watoto (2). Aidha, rufaa 11 zilifikishwa kwa Maafisa Ustawi wa Jamii na rufaa 32 kwenye Dawati la Jinsia na Watoto. Vilevile, watoto 329 waliopiga simu walipewa ushauri nasaha na elimu kuhusu ukatili.
Huduma za Ustawi kwa Watoto
85. Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali yakiwemo Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na Taasisi za Dini imeendelea kuratibu upatikanaji wa huduma za msingi za malazi, chakula, mavazi, matibabu na elimu kwa watoto walio katika mazingira hatarishi wanaoishi katika makao ya watoto yanayomilikiwa na Serikali na Taasisi Binafsi. Katika kipindi cha Julai 2018 hadi Machi 2019, jumla ya watoto 13,420 walipatiwa huduma za msingi katika makao ya watoto ikilinganishwa na watoto 6,132 waliokuwa kwenye makao kwa mwaka 2017/18. Nitumie fursa hii kupitia Bunge lako Tukufu kutoa wito kwa jamii kuzingatia misingi na utamanduni wa
18
kitanzania wa kutunza watoto, ndugu na jamaa zao ili kuepusha watoto kulelewa katika vituo.
86. Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI imeendelea kuwatambua na kuwezesha huduma za msingi kwa watoto wanaoishi mitaani. Jumla ya watoto 1,481,771 walio katika mazingira hatarishi walitambuliwa na kupatiwa huduma kama vile chakula, malazi, mavazi, matibabu na kuunganishwa na familia zao. Kati yao, watoto 930 waliwezeshwa kuunganishwa na familia zao.
Huduma za Ustawi kwa Wazee
87. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutoa huduma za msingi ikiwemo chakula, malazi, mavazi na matibabu kwa wazee wakiwemo wazee wasiojiweza wanaoishi katika makazi 17 ya wazee yanayomilikiwa na Serikali. Makazi hayo ni Kibirizi, Njoro, Kolandoto, Ngehe, Bukumbi, Ipuli, Fungafunga, Chazi, Mwanzange, Misufini, Nunge, Nyabange, Kilima, Sukamahela, Magugu, Nandanga na Nkaseka. Katika kipindi cha Julai 2018 hadi Machi 2019, jumla ya wazee wasiojiweza 510 wamepatiwa huduma. Aidha, Wizara ilitoa elimu na kuhamasisha jamii kulinda na kuheshimu haki za wazee kupitia majukwaa mbalimbali ikiwemo Maadhimisho ya Kimataifa ya Siku ya Wazee ya mwaka 2018 ambayo yalifanyika mwezi Oktoba 2018, Mkoani Arusha. Kaulimbiu kwa mwaka 2018 ilikuwa ‘Wazee ni Hazina ya Taifa: Tuenzi Juhudi za Kutetea Haki na Ustawi Wao’.
Huduma za Usuluhisho wa Migogoro ya Ndoa na Mashauri ya Matunzo ya Watoto
88. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kufanyia kazi mashauri ya migogoro ya ndoa na matunzo ya watoto kupitia Mabaraza ya Usuluhishi ya Ndoa katika ngazi ya Mikoa na Halmashauri ili watoto wapate haki za msingi kutoka kwa wazazi wao. Katika kipindi cha Julai 2018 hadi Machi 2019, jumla ya mashauri ya migogoro ya ndoa 16,832 yalipokelewa na kufanyiwa usuluhishi katika mikoa mbalimbali nchini ikilinganishwa na mashauri 13,382 yaliyofanyiwa kazi mwaka 2017/18 sawa na ongezeko la asilimia 26. Kati ya mashauri hayo yaliyopokelewa mwaka 2018/19, mashauri 14,035 yamesuluhishwa na kukamilika, mashauri 1,410 yamepelekwa mahakamani na mashauri 1,387 yanaendelea kufanyiwa usuluhishi kama inavyoonesha katika Kiambatanisho Na.19 cha hotuba yangu
Kukuza Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi
89. Mheshimiwa Spika, Uwezeshaji wanawake kiuchumi ni suala muhimu katika kufikia usawa wa kijinsia na kupunguza umaskini wa kipato katika jamii. Katika kufikia lengo hili, Serikali imeweka kipaumbele katika uwezeshaji wanawake kiuchumi kama mkakati wa kufikia usawa wa kijinsia katika nyanja zote. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Benki ya Posta Tanzania imeendelea kuwezesha wanawake kiuchumi kwa kutoa mikopo yenye masharti nafuu. Katika kipindi cha kuanzia Agosti 2018 hadi Machi 2019, Dirisha la Wanawake la Benki ya Posta Tanzania ambalo limeanzishwa ili kuendeleza huduma zilizokuwa zinatekelezwa na Benki ya Wanawake Tanzania limetoa mikopo yenye thamani ya shilingi 2,050,100,000.00 kwa wanawake wajasiriamali 3,035 kutoka katika mikoa 26 ya Tanzania Bara.
90. Mheshimiwa Spika, pamoja na uhamasishaji wa Wanawake kujiunga na vikundi vya kiuchumi, Wizara kwa kushirikiana na SIDO, TFDA, BRELA na TBS imeendelea kutoa mafunzo kwa wanawake ya kiuchumi kupitia stadi na mafunzo mbalimbali. Kwa mwaka 2018/19, jumla ya wanawake wajasiriamali 444 walipewa mafunzo kuhusu stadi za ujasiriamali, huduma ya hifadhi ya Jamii, fursa za kiuchumi, uboreshaji wa huduma na bidhaa zinazozalishwa na wanawake, teknolojia rahisi za uzalishaji wa bidhaa na urasimishaji wa biashara.
19
91. Mheshimiwa Spika, Ukatili wa kijinsia umeendelea kuwa tatizo katika jamii zetu ambapo wananchi wameendelea kuumizwa, kuteseka na hata kuuawa kutokana na vitendo vya ukatili vinavyofanyika hapa nchini. Katika kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia, Wizara kwa kushirikiana na wadau imeendelea kuratibu utekelezaji wa afua mbalimbali za kuelimisha na kuhamasisha jamii kushiriki katika jitihada za kutokomeza ukatili wa kijinsia. Elimu na uhamasishaji huo ulifanyika kupitia kampeni ya siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia ambayo ilizinduliwa na Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa (Mb.), Waziri Mkuu iliyoambatana na maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake Wanaoishi Vijijini, maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, makongamano, midahalo na mikutano mbalimbali.
Mashirika Yasiyo ya Kiserikali
92. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ili yachangie katika kuleta maendeleo kwa Taifa. Katika kipindi cha mwaka 2018 hadi Machi, 2019, jumla ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali 617 yamesajiliwa na kupatiwa cheti cha usajili ikilinganishwa na mashirika 385 yaliyosajiliwa mwaka 2017 sawa na ongezeko la asilimia 60. Kati ya mashirika 617 yaliyosajiliwa, mashirika 44 yamesajiliwa katika ngazi ya Kimataifa, mashirika 551 katika ngazi ya Kitaifa, mashirika 15 ngazi ya Wilaya na mashirika saba katika ngazi ya Mkoa kama inavyoonesha katika Kiambatisho Na. 21.
93. Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria, taratibu, mila na desturi za nchi, Wizara imewezesha kuandaliwa kwa Kanuni za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali za mwaka 2018 na kutangazwa katika Gazeti la Serikali Na.609 la tarehe 19 Oktoba, 2018. Kanuni hizi zinalenga kukuza uwazi na uwajibikaji wa mashirika kwa Serikali katika masuala ya fedha ambapo mashirika haya yanatakiwa kuweka wazi vyanzo vya fedha, kiasi kilichopatikana na utekelezaji wake.
F. UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA TAASISI ZILIZO CHINI YA IDARA KUU YA MAENDELEO YA JAMII
Utekelezaji wa majukumu ya Taasisi zilizo chini ya Fungu 53 umeainishwa kuanzia ukurasa wa 150 hadi 154 wa hotuba yangu.
Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru
94. Mheshimiwa Spika, Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru imeendelea kutoa mafunzo ya maendeleo ya jamii katika ngazi ya Astashahada, Stashahada, Shahada na Stashahada ya Uzamili. Katika mwaka 2018/19, Taasisi inatarajia kukusanya kiasi cha Sh.4,933,295,725.00 ambapo hadi Machi, 2019, Taasisi iliweza kukusanya Shilingi 2,841,681,722.00 sawa na asilimia 58 ya makadirio. Taasisi ilidahili jumla ya wanafunzi 1,183 katika fani ya maendeleo ya jamii ikilinganishwa na wanafunzi 743 waliodahiliwa mwaka 2017/18 sawa na ongezeko la asilimia 59.
Taasisi ya Ustawi wa Jamii
95. Mheshimiwa Spika, Taasisi ya Ustawi wa Jamii imeendelea kutoa mafunzo katika ngazi ya Astashahada, Stashahada, Shahada, Stashahada ya Uzamili na Shahada ya Uzamili. Katika mwaka 2018/19, Taasisi ilitarajia kukusanya kiasi cha Sh.10,403,984,423.00 ambapo hadi Machi, 2019, Taasisi iliweza kukusanya Sh.4,198,252,950.00 sawa na asilimia 40.35 ya makadirio.Taasisi ilidahili wanafunzi 1,064 ikilinganishwa nawanafunzi 1,185 waliodahiliwa mwaka 2017/18.
G. VIPAUMBELE VYA WIZARA NA BAJETI KWA MWAKA 2019/20
20
Vipaumbele vya Wizara yangu katika kipindi cha mwaka 2019/20 vimeainishwa kuanzia ukurasa wa 155 ukurasa wa 155 hadi 167 wa hotuba yangu.
IDARA KUU YA AFYA - FUNGU 52
96. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2019/20 Wizara kupitia Fungu 52 (Idara kuu ya Afya) imejiwekea vipaumbele vifuatavyo ili kuboresha huduma za afya nchini:
(i) Kuendelea kuimarisha na kuboresha utoaji wa huduma za chanjo ili kuwakinga watoto chini ya mwaka 1 dhidi ya magonjwa yanayozuilika kwa chanjo;
(ii) Kuendelea kuimarisha hali ya lishe na usafi wa mazingira ili kuwezesha wananchi kujikinga na magonjwa;
(iii) Kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa Tiba, vitendanishi katika vituo vya umma vya kutolea huduma za afya;
(iv) Kuendelea kuboresha huduma za Afya ya uzazi, mama na mtoto, ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wa chini ya miaka 5;
(v) Kuendelea na juhudi ya kupunguza pengo kati ya mahitaji halisi ya watumishi wa afya na idadi ya watumishi waliopo katika vituo vya umma vya kutolea huduma za afya;
(vi) Kuboresha Miundombinu na utoaji huduma katika Hospitali za Rufaa za mikoa;
(vii) Kuimarisha huduma za Kibingwa katika Hospitali za Taifa, Maalum na Kanda nchini;
(viii) Kuendelea na utekelezaji wa afua mbalimbali zenye lengo la kuimarisha na kupunguza maambukizo ya UKIMWI, TB na Malaria;
(ix) Kuendelea kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo, Saratani, Kisukari, Shinikizo la Damu na Magonjwa wa Moyo.
(x) Kuimarisha mifumo ya utoaji taarifa pamoja na ile ya Kielekitroniki katika Hospitali za Rufaa za Mikoa; na
(xi) Kukamilisha Mchakato wa maandalizi ya kutunga sheria ya Bima ya Afya itakayomtaka kila mwananchi kuwa na Bima ya Afya ikiwa ni mkakati mahususi wa kufikia lengo la Taifa la Afya kwa wote ifikapo mwaka 2030.
97. Mheshimiwa Spika, ili kutekeleza vipaumbele vilivyoanishwa katika mwaka 2019/2020, kazi zitakazotekelezwa ni pamoja na:
98. Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha 2019/2020, Wizara itaendelea kununua na kusambaza chanjo kulingana na mahitaji ya nchi kwa ajili ya kuwakinga watoto wa umri wa chini ya mwaka 1 na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo, ambapo jumla ya shilingi Bilioni 30 zimetengwa.
99. Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha 2019/2020, Wizara itaendelea kutekeleza afua mbalimbali za huduma ya Kinga ikiwa ni pamoja na Kupunguza Vifo vya akina Mama vitokanavyo na Uzazi na vifo vya Watoto ambapo jumla ya shilingi bilioni 5 zimetengwa. Kazi zilizopangwa kutekelezwa ni pamoja na ujenzi wa vituo 12 vya damu salama katika Mikoa 12 ya Dar Es Salaam, Mwanza, Morogoro, Geita, Kigoma, Mtwara, Mbeya, Tabora, Dodoma, Pwani, Arusha na Kagera pamoja na kazi hiyo pia kutafanyika upanuzi wa wodi za wazazi na kutenga vyumba vya wagonjwa Mahututi wanaotokana na uzazi katika hospitali za Rufaa za mikoa 5; Pia, ukarabati na ujenzi wa wodi maalum kwa ajili ya watoto wachanga utafanyika katika Hospitali za Rufaa za Mikoa 7.
100. Mheshimiwa Spika, ili kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza hususani Kisukari, magonjwa ya Moyo na Shinikizo la damu, Saratani na magonjwa Sugu ya njia ya hewa kama Pumu katika mwaka 2019/20 Wizara itaanzisha Mpango wa Taifa wa Kudhibiti
21
Magonjwa Yasiyoambukiza nchini ambapo afua mbalimbali zitatekelezwa kukabiliana na magonjwa haya.
101. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2019/2020 Wizara imejipanga Kuendelea na uboreshaji wa upatikanaji wa huduma za Dawa, Vifaa, Vifaa Tiba na Vitendanishi kwa kununua na kuvisambaza katika vituo vya kutolea Huduma za Afya vya Umma nchini. Jumla ya shilingi bilioni 200 zimetengwa.
102. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara imejipanga kuendelea na uboreshaji wa upatikanaji wa Damu salama katika vituo vya kutolea Huduma za Afya nchini ambapo imetenga jumla ya Shilingi Bilioni 2 zimetengwa
103. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2019/2020 Wizara itaendelea kuimarisha upatikanaji na utoaji wa huduma za matibabu ya kibingwa nchini kupitia Hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo kiasi cha Shilingi bilioni 4 kimetengwa Aidha, Wizara itaendelea kuimarisha huduma za kibingwa katika Taasisi ya Tiba ya Moyo Jakaya Kikwete ambapo kiasi cha Shilingi bilioni 1 kimetengwa. Shilingi bilioni 5 kimetengwa ili kuiwezesha MOI kuendelea kutoa huduma za matibabu ya kibingwa kwa maradhi ya mgongo, mishipa ya fahamu na mifupa, kuwaongezea ujuzi wataalam wa upasuaji, kununua vifaa na vifa tiba vya Kisasa.
104. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2019/2020 Taasisi ya Saratani Ocean Road itaendelea kuimarisha huduma za kinga, uchunguzi, mafunzo na tiba ya saratani ambapo jumla ya shilingi billion 1.7 zimetengwa.
IDARA KUU YA MAENDELEO YA JAMII - FUNGU 53
105. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2019/20, Wizara kupitia Fungu 53 itatekeleza vipaumbele vifuatavyo ili kuboresha utoaji huduma za ustawi wa jamii na maendeleo ya jamii:
(i) Kuamsha ari ya wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo;
(ii) Kukuza usawa wa jinsia na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi;
(iii) Kuimarisha upatikanaji wa haki na maendeleo ya mtoto;
(iv) Kuimarisha huduma za ustawi wa jamii kwa wazee na watoto walio katika mazingira hatarishi;
(v) Kuimarisha usimamizi na uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali;
(vi) Kuimarisha uratibu wa utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (2017/18 – 2021/22); na
(vii) Kuboresha mafunzo ya ustawi wa jamii na maendeleo ya jamii ili kuendelea kuzalisha wataalam wenye ubora kwa kufanya ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru, Vyuo vya Maendeleo ya Jamii, Taasisi ya Ustawi wa Jamii pamoja na Chuo cha Ustawi wa Jamii Kisangara.
H. SHUKRANI
106. Mheshimiwa Spika, Wizara imekuwa ikipata ushirikiano mkubwa kutoka nchi rafiki, Mashirika ya Kimataifa na sekta nyingine zinazosaidia na kuchangia katika huduma za Afya, Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii. Napenda kuchukua nafasi hii ya kipekee kuzishukuru nchi za Denmark (DANIDA), Uswisi (SDC), na Ireland (Irish
22
Aid), Canada (GAC), Korea Kusini (KOICA) na Mashirika ya Maendeleo ya Kimataifa yakiwemo Benki ya Dunia, UNICEF, kwa kuchangia katika Mfuko wa Afya wa Pamoja (Health Basket Fund), ambao umesaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma za afya nchini. Aidha, napenda kuzishukuru nchi za China, Cuba, India, Italia, Japan, Marekani, Misri, Sweden, Uingereza, Ujerumani na Ufaransa nan chi nyingine ambazo zimeendelea kuisaidia Wizara kwa njia mbalimbali katika kutekeleza majukumu yake.
107. Mheshimiwa Spika, vilevile nayashukuru mashirika mengine ya Kimataifa kwa ushirikiano wao waliotoa kwa Wizara pamoja na Wadau wa Maendeleo ambao kwa pamoja wamewezesha wizara yangu kutekeleza mikakati ya kisekta na hivyo kuboresha upatikanaji wa huduma za afya nchini Wadau wote hawa wameainishwa kwenye Hotuba yangu kuanzia aya ya 214 mpaka ya 216.
108. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha utendaji wangu wa kazi nikiwa Waziri, nimepata ushirikiano mkubwa kutoka kwa viongozi na wafanyakazi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Napenda kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile (Mb.), Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa ushirikiano mkubwa anaonipa katika kutekeleza majukumu yangu. Aidha, naomba kuwashukuru Dkt. Zainabu Chaula Katibu Mkuu (Afya) na Dkt John K. Jingu Katibu Mkuu (Maendeleo ya Jamii) kwa mchango wao katika kuwezesha utekelezaji wa majukumu yangu. Vilevile, nawashukuru Prof. Muhammad Bakari Kambi, Mganga Mkuu wa Serikali, Makamishna, Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo vya Wizara. Nawashukuru pia wakurugenzi wakuu wa hospitali za Taifa na Kanda ambao ni Prof. Lawrence M. Museru (Hospitali ya Taifa Muhimbili) Dr. Julieth Magandi (Hospitali ya Mloganzila), Dr. Respicious L. Boniface (Taasisi ya Mifupa MOI), Prof. Mohamed Janabi (Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete), Dr. Julius Mwaiselage, (Taasisi ya Saratani ya Ocean Road), Dr. Alphonce Chandika (Hospitali ya Benjamin Mkapa), Dr. Riziki M. Kisonga (Hospitali ya Kibong’oto), Dr. Erasmus E. Mdeme (Hospitali ya Mirembe) na Wakurugenzi wa Hospitali za Rufaa za Kanda Dr. Godlove Mbwanji (Hospitali ya Rufaa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Mbeya), Prof. Abel Makubi (Hospitali ya Bugando) na Dr.Gileard Masenga (Hospitali ya KCMC). Kipekee naomba kuwashukuru wakurugenzi na wakuu wa Taasisi zote zilizo chini ya Wizara ambazo ni MSD, NHIF, TFDA, NIMR, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, TFNC, Taasisi ya Ustawi wa Jamii, Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru pamoja na Mabaraza ya Kitaaluma na Bodi za Usajili, Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Waganga Wafawidhi wa Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati, Wakuu wa Vyuo vya Mafunzo vilivyo chini ya Wizara na wafanyakazi wote wa Wizara na Mashirika ya Dini, ya Kujitolea na Binafsi. Natoa shukrani kwa sekta zote ambazo tunashirikiana nazo katika kutoa huduma za afya, maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii pamoja na wananchi wote kwa ushirikiano wao. Nawaasa waendelee kuzingatia misingi ya huduma bora na kufanya kazi kwa bidii kwa manufaa ya taifa letu.
109. Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii pia kuishukuru familia yangu, kwa uvumilivu wao na pia kwa kunitia moyo katika kutekeleza majukumu yangu ya Kitaifa. Kwa wananchi wa Mkoa wa Tanga nawashukuru kwa ushirikiano wanaoendelea kunipatia katika kutekeleza majukumu yangu. Naahidi kuwa nitaendelea kuwaenzi na kuwatumikia kwa nguvu zangu zote ili kuleta mabadiliko ya haraka ya kimaendeleo katika Mkoa wetu.
I. MAOMBI YA FEDHA KWA KAZI ZILIZOPANGWA KUTEKELEZWA KATIKA MWAKA WA FEDHA 2019/20
Idara Kuu ya Afya - Fungu 52
23
Makadirio ya Makusanyo ya Maduhuli kwa Mwaka wa Fedha 2019/20
110. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2019/20 Wizara na Taasisi zilizo chini yake imekadiria kukusanya kiasi cha Shilingi Bilioni Mia Mbili Arobaini na Sita Milioni Mia Mbili Tisini na Nane Laki Sita Elfu Kumi na Saba Mia Nane na Themanini na Nne (246,298,617,884.00). Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Ishirini na Sita Milioni Thelathini na Moja Laki Sita Elfu Saba Mia Nane Ishirini na Saba (26,031,607,827.00) zinatarajiwa kukusanywa kutoka vyanzo vya ndani (Makao Makuu ya Wizara). Makusanyo hayo ni sawa na ongezeko la asilimia 24 ikilinganishwa na kiasi cha Shilingi Bilioni Kumi na Tisa Milioni Mia Saba Sabini na Tano Laki Nne Elfu Tisini na Nane Mia Moja (19,775,498,100.00) zilizoidhinishwa katika mwaka wa fedha 2018/2019. Aidha, Mashirika yaliyo chini ya Wizara yanakadiriwa kukusanya Shilingi Bilioni Mia Mbili Ishirini Milioni Mia Mbili Sitini na Saba Elfu Kumi na Hamsini na Saba (220,267,010,057).
Matumizi ya Kawaida
111. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2019/2020, Wizara kupitia (Fungu 52) imepanga kutumia kiasi cha Shilingi Bilioni Mia Nne Kumi na Tano Milioni Kumi na Nne Laki Mbili na Elfu Sitini na Mbili (415,014,262,000.00) ili iweze kutekeleza majukumu yake. Kati ya fedha hizo, kiasi cha Shilingi Bilioni Tisini na Tatu Milioni Mia Tisa Ishirini na Saba Laki Nane na Elfu Tisini (93,927,890,000.00) kwa ajili ya Matumizi ya kawaida, ambapo kiasi cha Shilingi Bilioni Mia Tatu Ishirini na Moja Milioni Themanini na Sita Laki Tatu na Elfu Sabini na Mbili (321,086,372,000.00) ni kwa ajili ya Mishahara ya Wizara na Taasisi zilizo chini yake.
Miradi ya Maendeleo
112. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa shughuli za maendeleo, Wizara (Fungu 52) inakadiria kutumia Shilingi Bilioni Mia Tano Arobaini na Nne Milioni Mia Moja Thelathini na Saba Laki Tisa Elfu Mbili Mia Tano na Tisini na Saba (544,137,902,597.00) kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo. Kati ya hizo, fedha za ndani ni Shilingi Bilioni Mia Mbili Sabini Milioni Mia Sita (270,600,000,000.00) ambayo ni sawa na asilimia 49.6 na fedha za nje ni Shilingi Bilioni Mia Mbili Sabini na Tatu Milioni Mia Tano Thelathini na Saba Laki Tisa Elfu Mbili Mia Tano Tisini na Saba (273,537,902,597.00) sawa na asilimia 51.4
113. Mheshimiwa Spika, Jumla ya Makadirio ya Bajeti kwa mwaka 2019/20 kwa Fungu 52 ni Shilingi Bilioni Mia Tisa Hamsini na Tisa Milioni Mia Moja Hamsini na Mbili Laki Moja Elfu Sitini na Nne Mia Tano Tisini na Saba (959,152,164,597.00)
Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii - Fungu 53
Makadirio ya Makusanyo ya Maduhuli kwa Mwaka wa Fedha 2019/20
114. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/20, Wizara imekadiria kukusanya Shilingi Bilioni Nne Milioni Mia Saba Sitini na Tatu Laki Tano na Elfu Tisini na Sita (4,763,596,000) kutokana na ada za wanafunzi kutoka Vyuo 8 vya Maendeleo ya Jamii na Chuo cha Ustawi wa Jamii Kisangara, ada ya usajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na mauzo ya vitabu vya zabuni.
Matumizi ya Kawaida
115. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/20, Wizara inakadiria kutumia kiasi cha Shilingi Bilioni Ishirini na Nane Milioni Mia Saba Sabini na Saba Laki Tatu na Elfu Sabini (28,777,370,000) kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida. Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Kumi na Mbili Milioni Mia Tisa Hamsini na Moja Laki Nane na Elfu Tisini na Mbili (12,951,892,000) ni Mishahara ya watumishi na Shilingi Bilioni Kumi
24
na Tano Milioni Mia Nane Ishirini na Tano Laki Nne na Elfu Sabini na Nane (15,825,478,000) ni Matumizi Mengineyo.
Miradi ya Maendeleo
116. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa shughuli za maendeleo, Wizara inakadiria kutumia Shilingi Bilioni Mbili Milioni Mia Saba Sitini Elfu Sitini na Moja na Kumi na Tatu (2,760,061,013) kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo. Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Moja (1,000,000,000) ni fedha za ndani na Shilingi Bilioni Moja Milioni Mia Saba Sitini Elfu Sitini na Moja na Kumi na Tatu (1,760,061,013) ni fedha za nje.
117. Mheshimiwa Spika, Jumla kuu ya fedha inayoombwa kwa mwaka 2019/20, kwa Fungu 53 ni Shilingi Bilioni Thelathini na Moja Milioni Mia Tano Thelathini na Saba Laki Nne Elfu Thelathini na Moja na Kumi na Tatu (31,537,431,013).
118. Mheshimiwa Spika, Jumla kuu ya fedha zote zinazoombwa kwa Wizara (Fungu 52 na 53) ni Shilingi Bilioni Mia Tisa Tisini Milioni Mia Sita Themanini na Tisa Laki Tano Elfu Tisini na Tano Mia Sita na Kumi (990,689,595,610.00). Kati ya fedha hizi shilingi Bilioni Mia Tano Arobaini na Sita Milioni Mia Nane Tisini na Saba Laki Tisa Elfu Sitini na Tatu Mia Sita na Kumi (546,897,963,610) ni kwa ajili ya maendeleo na shilingi Bilioni Mia Nne Arobaini na Tatu Milioni Mia Saba Elfu Tisini na Moja Laki Sita na Elfu Thelathini na Mbili (443,791,632,000) ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida.
119. Mheshimiwa Spika, Hotuba kamili inapatikana katika tovuti za Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto www.moh.go.tz. na www.mcdgc.go.tz.
120. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

Comments

Popular posts from this blog

Barua ya Kuomba Kazi

ANDIKO LA MRADI WA KUOMBA UFADHILI

Barua ya Maombi ya Kazi Kupitia Email (Barua Pepe)