LOWASSA ATANGAZA KUGOMBEA URAIS MWAKA 2020
LOWASSA ATANGAZA KUGOMBEA URAIS MWAKA 2020
Malunde Monday, July 17, 2017
Lowassa
aliyejitokeza kugombea urais kupitia CCM mwaka 2015 na jina lake
kukatwa kisha kuhamia Chadema alikogombea nafasi hiyo akiwakilisha vyama
vilivyoungana chini ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na kushindwa
na Rais John Magufuli, bado anatajwa kuwa mgombea mwenye nguvu katika
kambi ya upinzani.
Kwa
mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Rais Magufuli alishinda kwa
kupata kura 8,882,935 sawa na asilimia 58.46, huku Lowassa wa Chadema
akijipatia kura 6,072,848 sawa na asilimia 39.97 ya kura zote.
Akizungumza
jana katika mahojiano maalumu na waandishi wa Nation Media Group (NMG)
jijini Nairobi, Lowassa alisema, “Kwa mapenzi ya Mungu nitajaribu tena
mwaka 2020 na nitapita kwa mikono safi.”
Kama
ambavyo amekuwa akisema tangu aliposhindwa katika uchaguzi huo wa 2015,
pia jana Lowassa alisema licha ya kuendeshwa katika mfumo usioaminika,
hakutaka kuwashawishi wafuasi wake wamwage damu kwa kudai ushindi.
“Wafuasi
wangu walitaka tuingie mitaani kudai ushindi, lakini kulikuwa na
bunduki nyingi mikononi mwa wanajeshi. Niliogopeshwa na umwagikaji wa
damu. Sikutaka kuingia Ikulu kupitia damu za watu kwa sababu sistahili
hivyo,” alisema.
Hata
hivyo, alisema licha ya uchaguzi huo kutoaminika, bado anamheshimu Dk
Magufuli kama Rais, japo mbunge huyo wa zamani wa Monduli alikataa
kukubaliana na utendaji wa mkuu huyo wa nchi kwa kipindi alichokaa
madarakani.
“Hata
kama Dk Magufuli alichaguliwa katika mfumo usioaminika wa uchaguzi,
bado tunamheshimu kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Lowassa.
Alisema, “Utendaji
wa Rais Magufuli utaamuliwa na watu utakapofika mwisho wa muhula huu
mwaka 2020. Bora niwe makini katika hili nisije nikanukuliwa vibaya
nikaingia kwenye matatizo nitakaporudi nyumbani.”
Lowassa
ambaye hivi karibuni amekuwa akiripoti Makao Makuu ya Jeshi la Polisi
jijini Dar es Salaam kutokana na kauli yake kuhusu viongozi wa Jumuiya
ya Uamsho waliokamatwa mwaka 2012 huko Zanzibar, alilaani ukiukwaji wa
demokrasia akisema Chadema itakwenda mahakamani kudai haki ya kufanya
siasa.
“Kukataza
huko siasa ni kinyume cha demokrasia na haki, hata hivyo tunajitahidi
kujiimarisha. Tumeshalalamika serikalini kuondoa katazo hilo lakini bado
inajivuta miguu. Tunaweza kulazimika kwenda kutafuta msaada wa
Mahakama,” alisema.
Kuhusu
kamatakamata ya viongozi wa upinzani, Lowassa alisema licha ya kupata
zaidi ya kura milioni sita, ameshindwa hata kuwashukuru wananchi
waliompigia kura.
“Nilipata
kura milioni sita na siwezi kufanya mikutano hata ya kuwashukuru watu
kwa kunipigia kura. Hiyo si tu kinyume cha demokrasia, bali si haki,” alisema Lowassa.
Wakati
Jeshi la Polisi likikataza vyama vya upinzani kufanya mikutano ya
hadhara mwaka 2016, Rais Magufuli alisema wanasiasa waliochaguliwa
wanaweza kufanya mikutano kwenye majimbo yao.
Hata hivyo, bado baadhi ya mikutano ya ndani ya vyama hivyo imeendelea kuzuiwa na viongozi wa upinzani wakikamatwa.
Licha
ya kukiri kuwa ndani ya upinzani kuna changamoto nyingi, Lowassa
alisema kuna wakati anapata faraja kuwa upande huo wa siasa.
“Ni
uzoefu mzuri unaoendana na nyakati nzuri na ninafurahia uzoefu huo kwa
sababu mimi bado ni maarufu na nina wafuasi wengi. Kukataza shughuli za
siasa ni hatua ya kuninyamazisha,” alisema.
Lowassa
alisisitiza msimamo wa Chadema wa kumuunga mkono Rais wa Kenya, Uhuru
Kenyatta katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Agosti 8 akisema
kiongozi huyo ni chaguo sahihi kwa demokrasia za Kenya.
“Tumekuwa
na vikao halali kama chama na vya wazi na kukubaliana kumuunga mkono
Uhuru Kenyatta achaguliwe tena. Ni mtu mzuri anayeunga mkono Jumuiya ya
Afrika Mashariki na anaheshimu viongozi wa upinzani,” alisema.
Hata
hivyo, Lowassa aliyekwenda Kenya kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa Waziri
wa Usalama, Jenerali Joseph Nkaisery alifafanua kuwa uamuzi wa kiongozi
sahihi wa kuiongoza Kenya utafanywa na Wakenya wenyewe kwenye uchaguzi
wa Agosti.
Alipoulizwa
ni kwa nini Chadema imebadilisha mgombea wanayemuunga mkono katika
uchaguzi wa Kenya, kutoka kwa Raila Odinga wa Nasa, Lowassa alisema
amekuwa akimuunga mkono Kenyatta kwa muda mrefu.
Kabla
Lowassa hajajiunga na Chadema, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe
alishatangaza kumuunga mkono Odinga wakati huo akiwa Waziri Mkuu wa
Kenya.
Akizungumzia
kauli ya Lowassa kumuunga mkono Kenyatta, mmoja wa viongozi wa muungano
wa Nasa, Musalia Mudavadi alimtaka kiongozi huyo aache kuwaingilia
katika uchaguzi huo na badala yake apambane na Dk Magufuli Tanzania.
Comments
Post a Comment